Moshi. Moshi yatikiswa na mauaji. Hivi ndivyo unavyoweza kuelezea matukio matatu, likiwamo moja la kifo cha mwanafunzi na mawili ya mauaji yakiwamo ya mwanamke kudaiwa kuuawa na mwenza wake na mwili wake kuchomwa moto.
Mbali na tukio hilo lililotokea katika mji wa Himo, lakini limo tukio la mume kudaiwa kumuua mkewe kwa kumchoma kisu na baadaye kumjeruhi kwa kisu mwanawe mwenye umri wa wiki mbili, tukio ambalo limeibua pia simanzi.
Kuhusu kifo cha mwanafunzi, Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, linamshikilia kwa mahojiano, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bishop Alpha Memoria High School Moshi, Naaman Samwel, kutokana na kifo cha mwanafunzi wa kidato cha nne shuleni hapo, Walter Swai.
ALSO READ
ACT Wazalendo yazindua ahadi yake Zanzibar
SIASA 3 hours ago
Mbowe asubiriwa Mbeya, Sugu naye kuhudhuria
SIASA 3 hours ago
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alithibitisha kutokea kwa matukio hayo.
Utata mauaji ya mwanafunzi
Taarifa kutoka kwa ndugu wa mwanafunzi huyo anayejulikana kwa jina maarufu la Kelvine, zinadai kifo cha ndugu yao kina utata na wanaamini adhabu ya kipigo na ‘pushapu’ anayodaiwa kupewa shuleni hapo ndio ilisababisha kifo chake.
Vyanzo mbalimbali, vilidai mwanzoni mwa Februari 2023, mwanafunzi alipewa adhabu na walimu ambao hawajatajwa kwa majina, ambapo alipigwa mateke kwenye mbavu na kupiga pushapu hadi kushindwa kutembea.
Ingawa hakuna taarifa rasmi ya uchunguzi wa kifo cha marehemu ambayo imefanywa na kuwekwa wazi, taarifa za awali zinadai kipigo hicho kilisababisha marehemu kuvia damu kwenye sehemu za mbavu na kisha kutengeneza usaha.
Mama mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Neema, alidai baada ya adhabu hiyo, wameelezwa kuwa wanafunzi wenzake walimbeba na kumpeleka bwenini, ambapo hakuweza kuingia darasani kwa muda wa wiki moja.
“Tarehe 16.02.2023 ndio baba (baba wa mtoto) alipigiwa simu kuwa mtoto anaumwa. Alipotoka naye nje ya geti mtoto alimwambia shule ni mbaya inapiga sana watoto na kutesa hivyo akamuomba baba yake amhamishe,”alidai.
Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo ya Neema, baba wa mtoto alimsihi avumilie kwanza apate matibabu na akipona angemhamisha, na alimchukua hadi nyumbani kwake Arusha na kulala naye lakini usiku hali yake ya kiafya ilibadilika.
Kwa mujibu wa Neema, baba alimchukua mtoto na kumuwahisha Hospitali ya Mount Meru ya jijini Arusha ambapo alipelekwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) na kuwekewa mashine lakini baadaye alifariki dunia.
“Tulipokea taarifa ya msiba Jumapili (Februari 19,2023) lakini ni msiba uliotushtua na kutuletea utata, kwa sababu siku kadhaa kabla hajafa alisema alipigwa na mwalimu kwenye mbavu na pushup. Toka hapo hakuwa sawa,”alidai Neema.
Hata hivyo, Kamanda Maigwa alilieleza gazeti hili kuwa uchunguzi wa madaktari umebaini mapafu ya mwanafunzi huyo yalijaa maaji na ndio sababu ya kushindwa kupumua.
‘‘Kushindwa kupumua hakuna uhusiano na kupigwa, lakini tutachukua vipimo zaidi.. Tunamshikilia mwalimu mkuu kwa sababu ya malalamiko ya ndugu,’’ alisema.
Tukio la mauaji, kuchomwa moto
Katika tukio la Februari 19,2023, mwanamke ajulikanaye kwa Jina la Josephine Mngara (27) mkazi wa Mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi anadaiwa kuuawa na kisha mwili wake kuchomwa moto huku sababu zikielezwa ni wivu wa mapenzi.
Mama mzazi wa binti huyo, Theodora Msuya, aliliambia gazeti hili jana kuwa mwanaye huyo mara nyingi amekuwa na mgogoro na mumewe na alikuwa akimshauri aondoke nyumbani kwake kutokana na vipigo alivyokuwa akipata.
“Nimepata taarifa za mwanangu kutoka kwa majirani kwamba ameuawa. Nilifika eneo la tukio nilikuta hakuna kitu, majivu na mabaki ya mwili wake yalikuwa yamechukuliwa,”alieleza mama huyo katika mahojiano hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori alisema Jeshi la polisi Mkoani humo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo la mwanaamke kukutwa ameungulia ndani katika nyumba ambayo haikai mtu na uchunguzi wa tukio hilo umeanza.
“Polisi katika kuchunguza wamekuta kuna michirizi ya damu kutoka nyumba ya jirani kuelekea kwenye hiyo nyumba ambayo mtu ameungua,” alisema mkuu huyo wa wilaya na kuongeza kuwa:-
“Polisi wanaendelea nalo kuchunguza, taarifa za awali ni kwamba kwenye hiyo nyumba ambayo wamekuta michirizi ya damu huu mwili ambao umeungulia ni nyumba ya kijana ambaye alikuwa na uhusiano na huyo kijana wa kike,”
“Kupitia Jeshi letu la Polisi Kuna mambo mawili yanafanyika, moja ni kumtafuta huyo mtu ambaye nyumba yake imekutwa na michirizi ya damu kutoka kwenye nyumba yake mpaka sehemu ambayo mwili umekutwa umeungulia,”alisema.
“Pia polisi wanafanya uchunguzi wa kitaalmu kuona kama mwili ulioungua na sampuli za mama mzazi wa binti aliyetoa ripoti kwamba binti yake amepotea kama zinawiana, ili kubaini huyo aliyeungua ni binti yake Josephine,” aliongeza.
Imeandikwa na Daniel Mjema, Janet Joseph na Florah Temba