Dar es Salaam. Wakati aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum akikabidhi ofisi kwa Sheikh Walid Omar, utata umeibuka baada ya kutoweka baadhi ya samani zilizokuwamo katika ofisi hiyo.
Makabidhiano hayo ya ofisi kati ya Sheikh Walid anayekaimu nafasi hiyo na Sheikh Alhad, hayakufanyika katika ofisi ya mkoa badala yake yalifanyika kwenye ofisi ya Kadhi Mkuu.
Hata hivyo, Mwananchi lilimtafuta Sheikh Alhad kuzungumzia madai ya kutoweka kwa samani hizo ambaye alisema, “hilo si kweli, hiyo ofisi si ya Bakwata peke yake ( Baraza Kuu la Waislamu Tanzania), kuna taasisi ya amani na zingine, kwa hiyo wenye vitu vyao wamechukua.”
Katika makabidhiano hayo, baadhi ya viongozi hawakuruhusiwa kuingia kwenye ofisi aliyokuwa akiitumia Sheikh Alhad ambaye alitenguliwa nafasi yake Februari 2, mwaka huu na Mufti Aboubakar Zuberi baada ya kikao cha Baraza la Ulamaa kilichojadili sakata la mtaalamu wa tiba mbadala, Juma Mwaka na mkewe Queen Masanja juu ya hatima ya ndoa yao.
Baraza hilo lilikuja na uamuzi wa kutengua uamuzi wa baraza la mkoa liloivunja ndoa hiyo.
Awali, Queen alipeleka malalamiko yake katika ofisi za Bakwata akidai kutoelewana na mumewe huyo maarufu Dk Mwaka, hivyo kuomba apatiwe talaka na Kadhi wa Mkoa.
Januari 25 mwaka huu, ndipo Baraza la Masheikh la Mkoa liliketi kisha Sheikh Alhad alitangaza kuivunja ndoa hiyo.
Februari 2 mwaka huu, Baraza la Ulamaa nalo lilitangaza kutengua uamuzi huo uliotolewa na Baraza la Masheikh chini ya Sheikh Alhad.
Jana Sheikh Alhad alikabidhi ofisi hiyo kwa Kaimu Sheikh Walid mbele ya Mwenyekiti wa Bakwata, Sheikh Khamis Mataka na Katibu Mkuu wa Bakwata, Nuhu Mruma.
Wengine walioshuhudia makabidhiano hayo ni kadhi mkuu na katibu wake, kadhi wa mkoa na katibu wake.
Mwenyekiti Bakwata
Akizungumzia makabidhiano hayo kutofanyika ndani ya ofisi ya Sheikh wa Mkoa, Mwenyekiti wa Bakwata Sheikh Mataka alisema ndivyo katibu mkuu Mruma alivyoamua.
Alipotafutwa Mruma kuzungumzie hilo sambamba na kutoweka kwa samani za ofisi hiyo, simu iliita bila kupokewa kwa muda mrefu.
Kung’olewa kwa viyoyozi
Taarifa za kung’olewa kwa viyoyozi katika ofisi hizo zilianza kusambaa mapema jana katika mitandao ya kijamii.
Mwananchi lilipokuwa ofisini hapo, lilibaini kung’olewa kwa mashine za viyoyosi hivyo, vilivyokuwa vimesimikwa upande wa nyuma ya ofisi hiyo huku kukiwa na matundu.
Baadhi ya wanaofanya kazi hapo, waliozungumza kwa masharti ya kutotajwa jina gazetini, walisema viyoyozi hivyo vilivyokuwa viwili, viling’olewa tangu Jumapili usiku.
“Mpaka siku ya Jumapili mchana viyoyozi hivyo vilikuwepo, lakini tulipokuja Jumatatu asubuhi hatukuvikuta,” kilisema chanzo hicho.
Kaimu Sheikh Wahid alipoulizwa amekubalije kukabidhiwa ofisi inayodaiwa imeng’olewa viyoyozi na kuchukuliwa baadhi ya samani alisema, “AC na samani, kwangu ni vitu vidogo sana vya kuhangaika navyo kwa sasa, samahani sana mwandishi kwa kukujibu hivyo naomba mniache nifanye kazi kwanza.”
Makabidhiano
Awali, Sheikh Walid alisema hatakuwa na maneno mengi zaidi ya vitendo kwa kuwa Mungu ndiye aliyepanga ashike wadhifa huo.
“Hata hivyo, neno kubwa ambalo watu wanapaswa kujua ni kwamba, anayetoka ni Sheikh na anayeingia ni Sheikh, makabidhaoni haya ni utaratibu tu wa Bakwata,” alisema.
Naye Sheikh Alhad alisema alichokifanya ni historia kubwa imewekwa hasa kutokana na kadhia iliyotokea.
“Mwenyezi Mungu ndiye anayekadiria na analolitaka ndilo analolifanya, ninachotaka kusema, tumpe ushirikikano Sheikh Walid na mimi nitaendelea kumpa ushirikiano.”
Alisema uteuzi wa Sheikh Walid ni sahihi kwa sababu ni mtu sahihi na ni rafiki yake, hivyo wale wanaojaribu kuwatenganisha hawataweza na wanajuana kwa mambo mengi.
“Kwa hiyo, Sheikh Walid nakukaribisha Bakwata, Bakwata ina vishindo vingi, vumilia tujenge baraza letu mengi yatakukuta, mengi yatataokea, kama sisi tulivyoweza kuvumilia, kiongozi asipovumilia inakuwa ni mtihani kwa hiyo nakukabidhi ofisi hii,” alisema Sheikh Alhad.