Wanaouzia Wanafunzi ‘Dawa Mvuto wa Mapenzi’ Waondolewa


Wauzaji wa dawa za asili wakiwa nje ya mlango wa kuingilia katika Shule ya Sekondari Viwandani iliyopo jijini Dodoma. Picha na Habel Chidawali


Dodoma. Siku chache baada ya gazeti hili kuandika kuhusu biashara ya dawa za mapenzi kwa wanafunzi wa shule za Sekondari Viwandani na Dodoma, Serikali imewaondoa wafanyabiashara hao.


Jumatano ya wiki iliyopita gazeti hili liliandika habari ikieleza ‘dawa za mvuto wa mapenzi, nguvu za kiume zinavyowatesa wanafunzi’ habari ambayo iliibua hisia za watu na Serikali kuchukua hatua.


Awali, Mkurugenzi wa Jiji, Joseph Mafuru na Meya Profesa David Mwamfupe waliahidi kulifanyia kazi jambo hilo na kuwaondoa wafanyabiashara, ili kuwanusuru wanafunzi na vitendo viovu.

“Tumekusikia na katika hili naagiza mara moja wanaohusika waende wakalifanyie kazi maana kuna mambo ya kusubiri, lakini mengine ni ya kuchukua hatua mapema iwezekanvyo,” alisema Profesa Mwamfupe.


Miongozi mwa mambo yaliyotajwa kufanyika eneo hilo ilikuwa ni kwa wauza dawa hao kuwauzia wanafunzi dawa za kuongeza nguvu za kiume, shanga za kuvaa kiunoni kwa wanafunzi wa kike na pengine kuwapa dawa zilizotajwa kuwa na mvuto wa kupendeza mbele ya wavulana.


Jana, mmoja wa walimu wa Sekondari ya Viwandani ambaye awali alizungumza na gazeti hili alisema hali ni nzuri kwa siku tatu baada ya habari iliyoandika na gazeti hili kuwafikia wakubwa.


“Nilivyokuambia, mimi si msemaji wa shule nenda kwa Mkurugenzi, ila Mwananchi (gazeti) mlistahili zawadi, sisi tumehangaika bila mafanikio lakini mlipoandika walikuja na kuwaondoa kwa taratibu na hakuna dalili za kurudi maana viongozi wanapita kila siku hapa,” alisema mwalimu huyo.


Hata alipozungumzia kituo cha bajaji na bodaboda kilichopo jirani na shule, alisema kinaweza kuwa na faida na hasara kwao ingawa madhara yake si makubwa kama ilivyokuwa kwa wauza dawa.


Akizungumzia kituo cha bajaji ambazo zinasimama nyuma ya uzio wa kituo cha afya Makole karibu na lango la shule, Mganga Mkuu wa Jiji Dk Andrew Method alisema wanaosimama hapo hawajaruhusiwa na kwamba hata hospitali inaona ni kero.


Dk Method alisema licha ya kuwa waendesha vyombo hivyo hawapati madhara kwa kusimama eneo ambalo kuna kichomea taka, lakini uwepo hapo ni hatari.


Mtaalamu huyo wa afya alisema kwa namna yoyote uwepo wa kituo hicho ni matatizo na kuomba Serikali bila kutumia mabavu iwaelekeze waondoke eneo hilo na kutafutia maeneo mengine.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad