Wataalamu watoa hadhari kwa walaji wa kitimoto




WALAJI wa nyama ya nguruwe, maarufu  kitimoto wametakiwa kuchukua tahadhari baada ya utafiti kuonyesha katika kipindi cha mwaka mmoja, Tanzania inapoteza zaidi ya Sh. bilioni 19 kutokana na athari zinazotokana na minyoo tegu inayosababisha vifo.

Utafiti huo unaonyesha binadamu huambukizwa anapokula nyama ya nguruwe wanaofugwa nyumbani bila kufuata kanuni za ufugaji au wale wanaojitafutia chakula mtaani na madhara yake ni kupata ugonjwa wa kifafa na wengine kupoteza maisha.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Kisayansi (CYSTINET Africa), Prof. Helena Ngowi, alibainisha hayo jana jijini Dodoma wakati wa warsha ya kujadili mrejesho wa matokeo ya utafiti kuhusu namna ya kudhibiti minyoo hiyo.

"Ukiangalia hapa nchini, wagonjwa wa kifafa takribani 212 ya wagonjwa wote wa ugonjwa huo, utakuta wametokana na minyoo tegu ya nguruwe na kuigharimu jamii Sh. bilioni 12 kwa ajili ya matibabu na hasara ya Sh. bilioni saba kutokana na kutupwa kwa nyama ya nguruwe yenye maambukizi," alisema.

Prof. Ngowi alisema ripoti ya mwaka 2014 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) na Shirika la Afya Duniani (WHO), inaonyesha minyoo tegu ya nguruwe ni tishio namba moja kati ya magonjwa ya vimelea yanayoenezwa kwa njia ya chakula.


"Muhtasari huu wa matokeo umetokana na uchambuzi wa kina wa matokeo ya utafiti uliochapishwa katika kipindi cha miaka 26 hadi kufikia Desemba mwaka 2021, zikifadhiliwa na wafadhili mbalimbali, ikiwamo serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi," alisema.

Aliongeza kuwa licha ya utafiti mbalimbali kufanyika, ukiwamo uliofanyika mara 78 katika kipindi cha mwaka 1995 na 2021, bado kuna haja ya kufanya utafiti mwingine ili kubaini ukubwa wa tatizo na kutafuta suluhisho endelevu.

Alitaja baadhi ya utafiti uliofanyika ulihusu kiwango cha maambukizi kwa binadamu, maambukizi kwa nguruwe, mgongano wa magonjwa mengine, vichocheo vya maambukizi na madhara ya kiuchumi.


Mwingine aliutaja ulihusu kudhibiti maambukizi kwa binadamu, kudhibiti maambukizi kwa nguruwe, mikakati ya elimu kwa jamii pamoja na nyanja zingine ndogo.

Dk. Benard Ngowi ambaye ni Mtafiti na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Ndaki ya Afya na Sayansi Shirikishi Kampasi ya Mbeya alisema matokeo yanaonekana kwa binadamu katika hali mbili.

Alitaja ya kwanza ni ile ya binadamu anakuwa na mnyoo kamili kwenye utumbo na ya pili ni ile hatua ya kiluwiluwi kwenye misuli na ubongo.

"Mtu anapokuwa na kiluwiluwi hao kwenye misuli, wanakuwa kama mchelemchele, yaani vitu vyeupevyeupe kwenye nyama na vikiwa kwenye ubongo ndiyo huwa vinasababisha mtu kupata kifafa.


"Wakiwa minyoo tu kwenye utumbo wanasababisha mtu kupata dalili zisizo za kawaida na ugonjwa huo kama vile kupoteza hamu ya kula, tumbo kutokuwa vizuri kujisikia kuharisha lakini haarishi, yaani ni kama dalili za mtu mwingine mwenye minyoo ya kawaida," alisema.

Alisema takwimu nyingi ni zile za mnyoo ambayo inakuwa nje ya utumbo kama vile kwenye ubongo, misuli, moyo na chini ya ngozi huku zikitofautiana kati ya wilaya na wilaya.

Dk. Ngowi ambaye ni Mtafiti Mwandamizi katika Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu Kituo cha NIMR Muhimbili, alisema takwimu hizo zinapishana kulingana na namna jamii inavyofuga nguruwe.

Alisema ili kumaliza tatizo, wamehimiza kufuatwa kwa mapendekezo ya utafiti huo ambayo yamehimiza kukomesha ufugaji wa nguruwe wanaojitafutia chakula mitaani na kuwa na machinjio maalum ya nguruwe.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad