Dar es Salaam. Uongozi wa SportPesa mapema leo Februari Mosi, 2023, umetoa taarifa ya kusikitishwa na uongozi wa Yanga kukiuka makubaliano ya kimkataba na kuzindua jezi mpya zenye nembo ya mdhamini mwingine.
Mwananchi Digital imefanya jitihada ya kuutafuta uongozi wa Yanga kutolea ufafanuzi suala hilo na kumpata kiongozi mmoja wa juu ambaye hakutaka jina lake litajwe na kusema wameshangaa hatua ya wadhamini wao wakuu, SportPesa kulalamika juu ya uamuzi huo, na kwamba mapema waliwatafuta kwa nyakati tofauti na kuwaeleza juu ya nia yao hiyo.
Kiongozi huyo alisema kila hatua ya kuingia mkataba wa mechi sita na kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya Haier waliwajulisha SportPesa ingawa hawakuonyesha kukubaliana na mdhamini huyo.
"Tuliwatafuta mara nyingi kuanzia Novemba mwaka jana baada ya kufuzu hatua ya makundi, tukawaambia kimaandishi kwamba tunatafuta namna ya kuisaidia klabu kwa sababu kubwa kuwa wao hawataruhusiwa kikanuni.
"Wakatuambia tuwapelekee uthibitisho kwamba CAF hawairuhusu SportPesa, tukamtuma mtu wetu CAF akapewa uthibitisho huo na tukarudi na kuwasilisha kwao, hawakujibu, tukawakumbusha hawakujibu.
"Baada ya muda, mwaka huu mapema tukawajulisha kwamba bado tunawatambua wao kuwa wadhamini wetu wakuu, lakini tumepata mdhamini maalumu ambaye hana mgongano nao wa kimaslahi ili tumtumie kwenye hizi mechi sita tu za hatua ya makundi," alisema kiongozi huyo.
Yanga ilitambulisha jezi hizo Januari 30, 2023, ambazo zina mdhamini mpya kampuni ya vifaa vya nyumbani ya Haier, ambayo imesaini kumpa Yanga Sh1.5 bilioni kwa mechi za mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.