WINGA matata wa TP Mazembe, Philippe Kinzumbi, anatajwa kuwa katika rada za kujiunga na Yanga katika usajili ujao baada ya kuvutiwa na kiwango chake.
Juzi Jumapili baada ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika wakati Yanga ikiifunga TP Mazembe mabao 3-1, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, aliteta kwa siri sana na winga huyo.
Katika mchezo huo, winga huyo alikuwa tishio kwenye safu ya ulinzi ya Yanga baada ya kuonesha kiwango bora jambo ambalo Yanga wanaamini wakimpata, atawasaidia sana.
Kilichotokea baada ya mchezo huo kumalizika kwa Yanga kushinda mabao 3-1, Hersi alionekana kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam akizungumza na Kinzumbi.
Mazungumzo hayo yalichukua zaidi ya dakika tano kabla ya Hersi kuagana na winga huyo ambaye alielekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Hersi mara baada ya kuzungumza na Kinzumbi, alimfuata, Mukoko Tonombe ambaye aliwahi kuitumikia Yanga kabla ya kwenda TP Mazembe, wakazungumza kidogo.
Kinzumbi alipoulizwa walichozungumza na Injinia Hesri, alisema: “Tuliongea mambo kadhaa, lakini kikubwa zaidi ni pongezi tu.”
Yanga katika usajili wa dirisha dogo msimu huu, ilikuwa katika mipango ya kumsajili kiungo mshambuliaji anayetokea pembeni, ikashindikana, wakamsajili beki Mamadou Doumbia, mshambuliaji Kennedy Musonda na kiungo Mudathir Yahya.