Zitto Aanzisha Msako Pesa za ‘Plea Bargaining"



Dar es Salaam. Mjadala wa wapi yalipo mabilioni ya shilingi yaliyolipwa na watuhumiwa wa uhujumu uchumi kupitia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) umechukua sura mpya, kufuatia shinikizo la kutaka Jaji Mkuu, Ibrahim Juma na aliyekuwa DPP, Biswalo Mganga wawajibike kwa kushindwa kuchukua hatua stahiki.

Sakata hilo, ambalo limeibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, vyombo vya habari na mikusanyiko mingine limeanza kujielekeza kwenye kusaka ni nani hasa wanapaswa kuwajibika kwa kushughulika vibaya na suala hilo.

Haya yamekuja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuonyesha wasiwasi wake kuhusu ni kiasi gani na wapi zilipo fedha zilizokusanywa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kupitia utaratibu wa ‘plea bargaining.’

Rais Samia alisema Jumanne wiki hii wakati wa hafla ya kuwaapisha wajumbe wa Tume ya Kupitia na Kuboresha Taasisi za Haki Jinai, Dodoma, kuwa mfumo wa haki jinai nchini umevurugika.


Akigusia ukubwa wa tatizo, Rais Samia alielezea malalamiko mengi yanayoelekezwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuhusu wapi na kiasi gani cha fedha zilikusanywa chini ya utaratibu wa plea bargaining.

“Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kulikuwa na ngoma kubwa kidogo inachezwa, mpaka kukusanya fedha za wale wa plea bargaining. Pesa zile nyingine zinaonekana na nyingine hazionekani. Uki-trace (ukifuatilia) utaambiwa kuna akaunti China, sijui zimepelekwa pesa zipi. Tukatizame haya yote, kuna nini hasa kilichoikumba Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,” alisema Rais Samia.

Tangu aeleze wasiwasi huo, kumekuwa na mjadala na shinikizo kutoka kwa wanasiasa, wanasheria na watetezi wa haki za binadamu kutaka hatua stahiki zichukuliwe.


Jana, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kupitia taarifa kwa vyombo vya habari kuwa Jaji Mkuu na Biswalo wanapaswa kujiuzulu kwa kuwa madai ya ‘kuyeyuka’ kwa fedha za plea bargaining yalitokea wakati wao wakiwa wasimamizi wakuu wa eneo hilo.

“Kwa maelezo hayo ya Rais, aliyekuwa msimamizi mkuu wa muhimili wa haki ni Jaji Mkuu (Profesa Juma) ambaye hadi sasa yupo na Mganga alikuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

“Na sasa ufisadi unanukia, wawili hao hawana sifa tena ya kuendelea kutumikia nyadhifa za kisheria walizonazo sasa,” alisema Zitto na kusisitiza kuwa viongozi hao wanapaswa kujiuzulu kupisha uchunguzi na kuusitiri muhimili wa mahakama.

Akifafanua kwa nini amemhusisha Jaji Mkuu, Zitto alisema tangu Biswalo aanze kunyooshewa kidole hakuna hatua iliyochukuliwa na mkuu huyo wa mhimili wa haki nchini.


“Kwa kuwa hakuchukua hatua na sasa Biswalo ni Jaji ambaye yupo chini ya Jaji Mkuu, pamoja na kunyooshewa kidole hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi yake,” alieleza.

Zitto alisema Jaji Mkuu alipaswa mara moja aanze mchakato wa kumwondoa Mganga pale alipoanza kunyooshewa kidole.

“Uamuzi ni wake (Jaji Mkuu), ama aondoke na Biswalo au aanzishe mchakato wa kumuondoa katika nafasi aliyonayo. Hatumhukumu kwa makosa ya DPP, lakini kwa kuwa tayari ameshatia doa ndani ya mahakama kutomchukulia hatua ni sawa na kulikumbatia doa hilo,” alisema.

Biswalo alikuwa DPP wakati sheria ya majadiliano kati ya DPP na watuhumiwa wa makossa ya uhujumu uchumi ilipoanza kutekelezwa nchini mwaka 2019.


Alisimamia makubaliano mengi ambayo yaliwezesha kukusanywa kwa mabilioni ya shilingi kupitia akaunti maalumu iliyosimamiwa na Benki Kuu (BoT).

Mei mwaka juzi, Rais Samia alimwondoa Biswalo katika wadhifa huo na kumteua kuwa Jaji wa Mahakama Kuu baada ya kufanya uteuzi wa majaji saba wa Mahakama ya Rufani na wengine 21 wa Mahakama Kuu.

Alipotafutwa kuzungumzia madai ya Zitto, simu ya Mganga iliita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi haukujibiwa hadi tunakwenda mitamboni.

Madai ya Zitto yalimwibua Mkurugenzi wa Maboresho na Utetezi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe, pia alisema kuna haja ya kuwajibisha wote watakaoonekana walishiriki kwenye tuhuma hizo kupitia mchakato wa kisheria.

“Kwa namna Rais alivyoongea tuhuma zinaenda kwa Biswalo moja kwa moja, ndiye aliyesimamia plea bargaining, kuna uwezekano akawajibika lakini atawajibika kwa kazi alizozifanya kama DPP na si kama jaji,” alisema Massawe alipozungumza na Mwananchi.


Alisema si rahisi kumuunganisha Jaji Mkuu na tuhuma hizo kwa sababu majukumu yake wakati suala hilo likitokea hayakumpa nafasi ya kuliingilia moja kwa moja.

“Jaji Mkuu naona yuko mbali sana na suala hili, mahakama haikuwa inajua pesa zinalipwa wapi na haikuwa na mkono wa kisheria kuingilia. Sisi tulipeleka pesa BoT baada ya kupewa akaunti na DPP, hatukupewa hata control number (namba ya malipo ya Serikali),” alisema.

Hata Onesmo Ole Ngurumwa, mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) naye alizungumzia suala hilo akitaka uamuzi wa kuchukuliwa hatua kwa wawili hao uachiwe kwa Tume ya Maadili ya Mahakama.

“Tume ya maadili ya mahakama ndiyo yenye mamlaka hiyo na baada ya kupelekewa taarifa na ushahidi yenyewe ndiyo itaona hatua inayopaswa kuchukua dhidi ya mtumishi wake,” alisema.

Kuhusu Tume iliyoundwa na Rais kuchunguza mfumo wa haki jinai, Ole Ngurumwa alisema kama itabaini tuhuma dhidi ya jaji, taarifa hizo zitapelekwa katika tume hiyo.

“Huo ndiyo utaratibu unaostahili na unapaswa kufuatwa, kwa hiyo tuhuma zozote dhidi ya jaji yeyote zipelekwe pamoja na ushahidi katika tume hiyo,” alifafanua.

Mtazamo wa Ole Ngurumwa unaungwa mkono na wa Askofu Methodius Kilaini, msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki la Bukoba aliyesema Tume ya mahakama ndiyo yenye mamlaka dhidi ya watendaji wa muhimili huo.

“Haiwezekani kila mtu aamke aseme fulani ajiuzulu, hapana. Kila kitengo kina mamlaka yake ya kukidhibiti, ikitokea kuna makosa kitengo hicho kina wataalamu watakaoshughulikia na si mtu mmoja,” alisema.

Alipotafutwa kueleza iwapo kuna hatua zozote wanazotarajia kuzichukua, Msajili Mkuu wa Mahakama Tanzania, Wilbert Chuma alijibu yuko kikaoni na kuomba atafutwe baada ya nusu saa. Alipopigiwa tena, simu iliita bila kupokewa.

Utaratibu kuondolewa ujaji

Pamoja na maoni hayo ya wadau, suala la mtu kusimamishwa au kuondolewa wadhifa wa ujaji si jepesi kutokana na mchakato mrefu wa kisheria. Kundi hilo la watumishi ni miongoni mwa yale yenye kinga au ulinzi wa kikatiba.

Ibara ya 110 (5-8) ya Katiba ndiyo inayofafanua utaratibu wa kufuatwa dhidi ya jaji anayekabiliwa na tuhuma au tabia/mwenendo mbaya.

Kwa mujibu wa ibara hiyo, ili Rais amuondoe jaji madarakani au kumsimamisha anapaswa kuunda tume maalumu ya kumchunguza juu ya kile anachotuhumiwa au kulalamikiwa, kisha tume hiyo itamshauri kumuondoa au la.

Wakati akichunguzwa, jaji anayetuhumiwa atalazimika kusimama kutekeleza majukumu yake kupisha uchunguzi.

Ibara ndogo ya 5, sehemu ya kwanza inabainisha kuwa jaji anaweza kuondolewa katika madaraka hayo pamoja na sababu za kumuondoa.

Sababu hizo ni pamoja na kushindwa kutekeleza kazi yake kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote; au kwa sababu ya tabia mbaya inayoathiri maadili ya kazi ya jaji au sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

Hata hivyo, sehemu ya pili ya ibara hiyo inaweka ugumu unaomtofautisha jaji na watumishi wengine, ikieleza kuwa jaji hataondolewa kazini ila kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya 7 ambayo ndiyo inayozungumzia mapendekezo.

Ibara ndogo ya 6 ndiyo inayoelekeza Rais kuteua tume maalumu kumchunguza kwanza jaji huyo.

Sehemu (a) ya ibara hiyo ndogo ya 6 inasema Rais atateua Tume ambayo itakuwa na mwenyekiti na wajumbe wengine wasiopungua wawili.

Mwenyekiti na angalau nusu ya wajumbe wengine wa tume hiyo itabidi wawe majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani katika nchi yoyote iliyomo kwenye Jumuiya ya Madola.

Sehemu (b) ya ibara hiyo ndogo ya 6 inaeleza kuwa tume hiyo itachunguza shauri lote na kutoa taarifa kwa Rais kuhusu maelezo ya shauri lote.

Baada ya hapo, tume hiyo itapendekeza iwapo jaji huyo aondolewe kazini kwa kushindwa kufanya kazi kutokana na maradhi au sababu nyingine yoyote au kwa sababu ya tabia mbaya.

Ibara ndogo ya 7 sasa ndiyo inaeleza kuwa ikiwa tume hiyo itapendekeza Jaji aondolewe ndipo Rais atamwondoa kazini kiongozi huyo.

Pia, Rais anaweza wakati wowote kufuta uamuzi huo wa kumsimamisha kazi jaji huyo na kwa hali yoyote uamuzi huo utabatilika ikiwa tume itamshauri Rais kwamba jaji huyo asiondolewe kazini.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad