KUNA wachezaji wawili pale Yanga walikuwa gumzo kubwa wakati waliposajiliwa ambao ni kiungo mshambuliaji Steohane Aziz Ki na beki wa kati Mamadou Doumbia.
Aziz Ki alisajiliwa akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast wakati Doumbia yeye alinaswa kutoka timu ya Stade Malien ya Mali.
Wakati tunapiga stori kijiweni tukawakumbuka wachezaji hao wawili kipindi hiki ambacho Yanga inafanya vizuri katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Huyu Aziz Ki licha ya kuanza vizuri alipoingia nchini, kwa sasa amekuwa akisugua benchi huku Doumbia tangu amekuja ameonekana kushindwa kulishawishi benchi la ufundi kumpa nafasi na mechi alizocheza hadi sasa hazizidi mbili.
Hata hivyo, licha ya wachezaji hao kutocheza, hakuna shabiki wa Yanga ambaye anaonekana kushtuka au kulalamika kwa nini hawapangwi. Wanayanga wanafurahi tu matokeo ya timu yao na hawajali kama Doumbia na Aziz Ki wanapangwa au wanasotea benchi.
Hii ni kwa sababu timu yao inapata matokeo mazuri. Mara zote Yanga wamekuwa wakijali zaidi timu yao kufanya vizuri kuliko mafanikio ya mchezaji mmojammoja.
Ni rahisi kwa Wanayanga kumshambulia kocha au kiongozi ikiwa mchezaji au wachezaji fulani hawachezi huku timu ikiwa haifanyi vizuri lakini inapotokea inafanya vizuri, timu hupewa kipaumbele kwanza kuliko mtu.
Ingekuwa balaa kubwa kwa Nasreddine Nabi na benchi lake la ufundi kama wangekuwa hawafanyi vizuri huku Aziz Ki na Doumbia wakiwa hawachezi lakini kwa vile Yanga inashinda na mashabiki wanatamba mtaani, hata hakuna anayepiga kelele.
Doumbia na Aziz Ki washukuru Yanga inafanya vizuri vinginevyo kwa ninavyowafahamu Wanayanga, sasa hivi kingekuwa kinawaka pale.