Atangaza kununua kila goli Simba, Yanga CAF



MDAU wa michezo ambaye pia ni shabiki na mwanachama wa klabu ya Yanga kutoka mjini Geita, Hussein Mwananyanzara ametangaza kununua kila goli litakalofungwa na timu za Simba na Yanga kwenye michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Ameahidi kwa kila goli litakalofungwa atatoa Sh 500,000  kwa mfungaji kama sehemu ya kuunga mkono zawadi ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyeahidi Sh milioni tano kwa kila goli litakalofungwa na timu hizo kwenye mashindano hayo.

Mwananyanzara ametoa ahadi hiyo  leo mbele ya waandishi wa habari na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita. Simba kesho itacheza dhidi ya Vipers ya Uganda Ligi ya Mabingwa Afrika na siku inayofuata Yanga itaivaa Real Bamako Kombe la Shirikisho, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Amesema matamanio yake kama ilivyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuona klabu za Tanzania zinafanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa na kukuza sekta ya michezo nchini.


“Kazi anayoifanya mama imenifurahisha, kwa hiyo na mimi nimeguswa, pamoja na kwamba mimi ni shabiki wa Yanga, lakini sitabagua timu,” alisema.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita,  Nicolous Kasendamila amepongeza hatua hiyo kwani inaunga mkono maono ya Mwenyekiti wa CCM Taifa kuendelea kukuza sekta ya michezo.

“Nitoe wito kwa wafanyabiashara wengine, wajitokeze kuhamasisha timu zetu, kwani tunatamani timu zetu zifanye vizuri, zifunge magoli mengi, ili ziweze kuchukua ubingw,” amesema.


Katibu wa CCM mkoa wa Geita, Alexandrina Katabi amewaomba wadau wengine kujitokeza kutoa hamasa kwa timu zingine za mkoani Geita ikiwemo Geita Gold, ili ziendelee kufanya vizuri zaidi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad