Baleke Noma Aiteka Mechi ya Mtibwa vs Simba, Atupia Bao Tatu Mwenyewe


Mshambuliaji wa Simba, Jean Baleke amefunga hat-trick ya kwanza kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu na kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Manungu Complex Morogoro.


Baleke aliyejiunga na timu hiyo dirisha dogo la Januari akitokea Nejmeh FC ya Lebanon alifunga mabao yote katika kipindi cha kwanza dakika ya 3, 7 na 36.


Hizi ndizo dondoo muhimu za mchezo huo.


Hat-Trick ya Baleke inakuwa ni ya sita kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu huku nyota wengine waliofunga wakiwa ni Fiston Mayele (Yanga) dhidi ya Singida Big Stars Novemba 17 mwaka jana, John Bocco akifunga mbili akianza na Ruvu Shooting Novemba 19, mwaka jana kisha Tanzania Prisons Desemba 30, mwaka jana.


Wengine waliofunga ni Saidi Ntibanzokiza 'Saido' wa Simba dhidi ya Tanzania Prisons Desemba 30, mwaka jana na Ibrahim Alli 'Mkoko' wa Namungo na KMC Januari 24, mwaka huu.


Mabao aliyofunga Baleke yanamfanya nyota huyo kufikisha matano hadi sasa baada ya awali kufunga dhidi ya Dodoma Jiji Januari 22 na Singida Big Stars Februari 3, mwaka huu.


Mtibwa imeendeleza uteja mbele ya Simba kwani mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Oktoba 30, mwaka jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ilikubali kichapo kizito cha mabao 5-0.


Mara ya mwisho kwa Mtibwa kuifunga Simba ilikuwa ni ushindi wa bao 1-0 ilioupata Februari 24 mwaka 2013 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.


Kichapo hiki kinaifanya Mtibwa kupoteza mechi ya 10 katika michezo 25 ambapo kati ya hiyo imeshinda saba na kutoa sare minane ikiwa nafasi ya tisa na pointi 29.


Kwa upande wa Simba inaendelea kusalia nafasi ya pili na pointi 57 katika michezo 24 iliyocheza ambapo kati ya hiyo imeshinda 17, sare sita na kupoteza mmoja tu.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad