Benchi la ufundi la Uganda limekiri kuwa lina kazi kubwa ya kufanya kupata bao dhidi ya Taifa Stars kesho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 2:00 kutokana na ubora wa safu ya ulinzi ambao wenyeji wao wamekuwa nao.
Mchezo huo ni wa marudiano wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zitakazofanyika Ivory Coast mwakani baada ya ule wa kwanza baina yao uliofanyika Machi 24 huko Misri ambao Taifa Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Baada ya kupoteza mchezo wa kwanza, Uganda inahitaji ushindi katika mechi ya leo ili iweke hai matumaini yake ya kufuzu Afcon lakini kama itapoteza, ndoto zake za kutinga fainali hizo itafutika rasmi na hata matokeo ya sare yatawaweka katika nafasi finyu ya kwenda Ivory Coast mwakani.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kocha wa Uganda 'The Cranes', Milutin Sredojevic 'Micho' alisema kuwa wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi ya kesho lakini hofu yao kubwa ni ubora wa Taifa Stars katika kujilinda.
"Ni vigumu kufanya transition (mabadiliko) dhidi ya timu yenye nidhamu kubwa ya kujilinda, yenye mabeki watatu wa kati, jumlisha Novatus (Dismas), jumlisha Himdi Mao na Mudathir Yahya. Ilikuwa ngumu kwetu kuvunja ukuta huo na sasa kuna Shomari (Kapombe) na Tshabalala (Mohammed Hussein)."
"Tuna wachezaji wachache waandamizi ambao wanaongoza mabadiliko ya kizazi na tunategemea zaidi kizazi kilichoshiriki Afcon U20 kule Mauritania. Hakuna mahali pazuri pa kumbadilisha mtoto kuwa mwanaume zaidi ya Benjamin Mkapa," alisema Micho.