Chadema, ACT Wazalendo wafunguka kualikwa CCM



Chama cha ACT-Wazalendo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), vimesema siri ya wao kushiriki katika maadhimisho ya miaka miwili ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan yaliyoandaliwa na Chama cha Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) ni maridhiano yanayoonyeshwa na kiongozi huyo.


Wakitoa maoni yao kuhusu mkutano huo, wachambuzi wa siasa wamesema kuwa kujumuika kwa pamoja kwa wanasiasa hao ni jambo jema ambalo linawaweka watu pamoja, kuliko kuishi kwenye chuki na uhasama.


Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika juzi washiriki wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa walialikwa wakiwamo wa Chama cha ACT-Wazalendo na CHADEMA.


Akizungumza na Nipashe kuhusu ushiriki wa wanawake wa chama chao katika maadhimisho hayo, Katibu Mkuu ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, alisema walifanya hivyo kwa kuzingatia mambo matatu.


Alisema moja ya sababu zilizowasukuma kuruhusu wanawake wa chama chao kushiriki ni kutokana na siasa za maridhiano zinazoonyeshwa na Rais Samia.


Sababu nyingine alisema ni kumpa moyo Rais Samia katika ahadi yake aliyoitoa ya Katiba mpya, Tume huru ya uchaguzi na mageuzi ya kisiasa kwa ujumla.


Kwa mujibu wa Ado, alisema ya tatu ni kuonyesha ushiriki wao katika msukumo wa ajenda ya mwanamke katika kupambana dhidi ya vikwazo vyote ambayo vinawakumba wanawake nchini.


“Sisi tumeshiriki tukio la kilele cha maadhimisho ya miaka miwili ya Rais Samia madarakani kwa sababu ya siasa za maridhiano ambazo amezikubali kuwa ndizo zinazoongoza duru za kisiasa hivi sasa na zinabadilisha pia mahusiano baina ya vyama,” alisema Ado.


“Tunaona Rais Samia mwenyewe anashiriki shughuli za vyama. Kwa mfano hivi karibuni alishiriki tukio la BAWACHA, hiyo inaongeza chachu kwa vyama kuendelea kushirikiana kwenye matukio. Haina maana kwamba tunaunga mkono lengo la tukio husika ila tunakwenda kuonyesha mshikamano na maridhiano ya kisiasa.


“Lakini tunashiriki katika matukio haya kumpa moyo Rais juu ya ahadi yake aliyoitoa ya Katiba mpya, Tume Huru ya Uchaguzi na mageuzi ya kisiasa kwa ujumla wake. Tunamwonyesha kwamba tuko pamoja kwenye hilo na tutashirikiana kujenga Tanzania mpya, kufungua ukurasa mpya.


“Na tuliwaruhusu wanawake ili kuonyesha ushiriki wetu katika msukumo wa ajenda ya mwanamke katika kupambana dhidi ya vikwazo vyote, ambayo vinawakumba wanawake na kuonyesha kwamba tuko tayari kushirikiana nje ya vyama vya siasa kwa ajili ya mustakabali mwema wa mwanamke wa ushirikishwaji na kuinuliwa kwao kisiasa, kiuchumi na kijamii.”


Kaimu Mwenyekiti wa BAWACHA, Sharifa Suleiman, alisema suala la vyama vya siasa kualikana kwenye matukio ni jambo la kawaida kwa ujenzi wa demokrasia.


“Sisi BAWACHA tulimwalika Rais wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake tuliyoiandaa na kuhudhuria. Kwa hiyo, kualikwa kwetu ni matokeo ya maadhimisho hayo. Ni jambo jema kualikana kwasababu sisi kama chama cha siasa hatuna ugomvi na chama tawala na vyama vyingine kwa sababu CHADEMA tuna dhamira ya kuliongoza taifa bila ubaguzi,” alisema.


“Lakini kimsingi hali hii imetokana na kufunguliwa kwa ukurasa mpya wa siasa kwa vyama vyetu kupitia maendeleo ya mazungumzo ya maridhiano yanayoendelea baina ya chama chetu na serikali kwa pamoja na chama kinachoongoza serikali yaani CCM.


“Kwa kifupi siri ya mafanikio haya ni mazungumzo ya maridhiano baina ya vyama vyetu na serikali inayoongozwa na Rais Samia na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman. Kinana kwa upande mmoja na Mwenyekiti wetu wa chama chetu taifa, Freeman Mbowe.”


Mjumbe wa kikosi kazi ngome ya ACT-Wazalendo Taifa, Halima Ibrahim Mohammed, alisema jambo kubwa lililowasukuma wao kushiriki ni namna wanavyoona mabadiliko anayoyaleta Rais Samia hususani katika kuonyesha kwamba siasa si uhasama.


“Tumeona mabadiliko kwa Rais Samia, hakuna jambo zuri kama nchi kuwa na amani, anaweka mazingira ya siasa yasiwe ya uhasama, chuki. Hilo ni jambo jema kwa sababu hii nchi ni yetu sote,” alisema.


Naye mchambuzi wa masuala ya siasa, Nassoro Kitunda, alisema kilichofanyika juzi kwa wanawake kukutana bila kuangalia vyama vyao vya siasa ni jambo jema na ndivyo inatakiwa kuwa badala ya kuwekeana chuki.


Pia alisema anaamini kwamba hali hiyo imetokana na utayari wa Rais Samia wa kutaka maridhiano.


“Tulikuwa tunahitaji kuwa na siasa za namna hii. Siasa za kukaa pamoja na kuzungumza masuala na siyo kukashifiana au kurushiana lugha zisizo na staha. Tunahitaji siasa za kushindana kwa hoja na ushawishi, kwa hiyo kilichofanyika katika tukio la jana (juzi) kwa wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa kukaa pamoja ni jambo jema sana,”alisema.


“Hatusemi kwamba siasa za namna hiyo zimeisha, lakini hata huu mwanzo ni mwema na hali hii imetokana na Rais Samia mwenyewe kuonyesha nia hiyo na kuwachukulia vyama vingine kwamba sio wapinzani bali ni vya kusaidia katika kuibua hoja na ndio maana hata wao wapinzani wamepata amani kushiriki.”


Alisema ni vema maridhiano yanayofanywa kwa vyama vya siasa na serikali yakafanywa pia na kwa wananchi kwa kuhakikisha wanasikilizwa na kutatuliwa changamoto zote zinazowasumbua.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad