MSHAMBULIAJI wa Yanga, Fiston Kalala Mayele, amesema wanachotakiwa kukifanya mashabiki wa timu hiyo ni kuhakikisha wanajaa katika Uwanja wa Mkapa, kisha suala la ushindi waliache kwao.
Kauli ya Mayele imekuja wakati leo Yanga ikiwa mwenyeji wa US Monastir, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika Kundi D utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
Mayele katika kikosi cha Yanga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, amefanikiwa kufunga mabao mawili, yote akiwatungua Real Bamako, ugenini na nyumbani.
Akizungumza na Spoti Xtra, Mayele alisema kuwa: “Kinachotakiwa kufanywa na mashabiki wa Yanga ni kuhakikisha wanakuja kwa wingi uwanjani na suala la ushindi watuachie sisi wachezaji tuwafurahishe.
“Huu ni mchezo ambao utatuheshimisha sisi kwa namna moja ama nyingine jambo ambalo wachezaji wote wameapa kuitafutia ushindi timu.
“Viongozi tayari wametuahidi mambo mazuri, lakini hata sisi tunataka kuweka rekodi yetu msimu huu katika michuano ya kimataifa, hivyo tutalipambania hilo.”
Naye mshambuliaji wa Yanga, Kennedy Musonda, alisema: “Mchezo huu ni muhimu sana kwetu, hakuna kingine ambacho tunahitaji zaidi ya usindi, tunawaahidi hilo mashabiki zetu.”
STORI: MARCO MZUMBE