Hakuna Namna Mastaa Lazima Wapumzike Taifa Stars

 


Usiku wa Jummane katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ilijiweka pagumu kupata tiketi ya Afcon mara baada ya kuruhusu kufungwa bao 1-0 na Uganda katika dakika za majeruhi.


Mara baada mchezo huo haishangazi kwa mashabiki wa Simba na Yanga kunangana katika vijiwe vya soka wakionyeshea vidole baadhi ya wachezaji kuwa ndio chanzo cha Stars kufungwa.


Moja ya ukosoaji wao ni kuwa baadhi ya mastaa wanajituma zaidi katika klabu kuliko timu ya taifa na pengine wapo mastaa wanaochoka kutokana na kutumika sana katika klabu na timu ya Taifa.


Ni kawaida kusikia maneno kama hayo kwa mashabiki hii ni kutokana na hali ya kughadhabika wanayoipata hasa wanapokosa matokeo mazuri wanayotarajia.


Iwe ni mchezaji wa Yanga au Simba ambao wana majukumu mengi ikiwamo yale ya klabu bingwa Afrika kwa Wekundu wa Msimbazi na Wakijani wa Jangwani ambao wako Kombe la Shirikisho lakini linapokuja jukumu la timu ya taifa hakuna namna wataitwa tu.


Si hao tu, hata kina Samatta, Msuva na wengine wanaocheza ligi kubwa na ngumu nao pia hakuna jinsi wataitwa na watatumika kote kote yaani katika klabu zao na timu Taifa.


Hata katika mchezo kuwania kufuzu kwa bara la Ulaya UEFA Euro 2023, ambapo Hispania ililala 2-0 dhidi ya Scotland ikiwa ina wachezaji wa klabu ya Madrid ambayo imetinga nusu fainali UEFA lakini nao walikuwemo akiwamo beki muhimu wa kulia Carvajal.


Katika kuyasaka mafanikio ya soka ya timu za Taifa hakuna namna mastaa wakali wanaoutumika sana katika klabu na timu ya Taifa wataitwa tu kusaidia kusaka mafaniko hayo.


Kutokana na wanasoka hawa wote kutumika mara kwa mara bila kupumzishwa inawaweka katika hatari ya kupata majeraha kirahisi au kuchoka katika mechi zilizokaribiana kama hizi zilizochezwa wiki hii na kuachana siku chache.


Ni kawaida wanasoka wenye kiwango cha juu kutumika na klabu zao na timu za taifa ingawa wanaweza kukupa matokeo mazuri kama tu hawana vijeraha au mchoko uliotokana na kutumika sana.


Nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta na nahodha wa Uganda Emmanuel Okwi walipumzishwa kipindi cha pili katika pambano hilo, hii ilikuwa ni mbinu nzuri kwa wachezaji wanaotumika sana kote kote.


Hii inawasaidia kupona majeraha ya ndani kwa ndani na pia kuondoka na uchovu wa misuli ingawa kwa upande mwingine inaweza kuwa hasara kwa timu kwani inapunguzia tishio kwa wapinzani.


Ni kawaida kwa wanasoka wengi wa aina hii kupata majeraha ya mara kwa mara kirahisi kutokana na tatizo la kuchezeshwa kila mara bila hata ya kupata mapumziko.


Vilevile kufanyishwa mazoezi magumu kupita kiasi bila kuzingatia ushauri tiba wa kuwapumzisha wanasoka kila wanapotoka katika mechi ngumu.


Pamoja na magumu yote wanayopata wanasoka hawa ila ndio vile hakuna namna wanatumika kote kote kuleta mafaniko katika timu za taifa na klabu.


MADHARA WANAYOPATA NI HAYA


Moja ya madhara wanayoyapata ni kupata majeraha ya kirahisi mara kwa mara hii ni kutokana na miili yao kukosa nafasi ya kupumzishwa ili kukabiliana na vijeraha vidogovidogo vya ndani kwa ndani.


Pamoja ya kwamba tishu za mwili wa binadamu hufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa sana lakini pale zinapofanyishwa kazi kupita kiasi huweza kuwa chanzo cha wanasoka wa aina hii kupata majeraha.


Kadiri mwili unavyotumikishwa ndivyo pia unakuwa katika hatari zaidi ya kupata majeraha mbalimbali ikiwamo ya misuli, mifupa na nyuzi ngumu yaani ligamenti na tendoni.


Ili mchezaji kuweza kumudu jambo hili umri alionao una maana kubwa, wanasoka wanapofikisha umri zaidi ya miaka 30 tayari mwili unakosa uimara ukilinganisha wanapokuwa na umri wa miaka 17-30.


Wachezaji wanapotumika sana miili yao huweza kuambatana na majeraha wakati wanashiriki mazoezi na mashindano mbalimbali kama haya ya AFCON na UEFA Euro.


Wachezaji wanaposhiriki mazoezi magumu kwa muda mrefu au kuchezeshwa michezo mingi bila kupumzishwa hukumbwa na vijeraha na mchoko wa misuli.


Kuyapuuzia majeraha madogo wanayopata, mbinu dhaifu za mazoezi na dosari za programu za mazoezi wanayofanya huchangia kupata majeraha kirahisi.


Majeraha haya hutokana na mrundikano wa magonjwa yakujirudia mara kwa mara katika tishu za mwili na kisha hapo baadaye jeraha hilo huongezeka ukubwa.


Pengine alipata jeraha katika mechi za kimataifa lakini hakupewa nafasi ya kupumzika majuma kadhaa ili kupona kabisa, baadaye anaposhiriki ligi ngumu ngazi ya klabu hujijeruhi zaidi.


Misuli na tishu nyingine mwilini zinapotumika sana huweza kujitengenezea mazingira ya kukabiliana na hali hiyo ikiwamo mbinu mpya za ukarabati wa jeraha na uponaji.


Mwili unapokuwa katika shinikizo kubwa na huku muda ukizidi kuyoyoma huweza kuongeza jeraha juu ya jeraha.


Mambo yanayoweka shinikizo kubwa katika jeraha au tishu ni pamoja kupigwa, kugandamizwa, kupindwa, kuvutwa, kujikunja na kupata mtetemo.


Hali hii huweza kuleta uchovu katika nyuzi ngumu za tendoni ambazo ni miishilio ya misuli ipachikayo mfupani, nyuzi ngumu za ligamenti zinazounganisha mfupa mmoja na mwingine, mishipa ya fahamu pamoja na tishu nyingine laini.


Matokeo yake ni kutokea kwa mabadiliko katika tishu hizo ili kujihami na kujiponya na uwepo wa mashinikizo ya mara kwa mara mwilini.


Uchovu katika tishu hizo ndio unaodhaniwa kuleta mabadiliko ya kujihami kwa tishu za mwili ili kukabiliana hali hiyo ya shinikizo la mara kwa mara katika hatua za awali.


Tishu za mwilini zinapojaribu kujitengenezea mazingira mapya kutokana na shinikizo lililopo majeraha yanaweza kujitokeza wakati huo labda tu iwe tishu hiyo imepona kabisa na jeraha kuunga kabisa.


Kifupi ni, kasi ya kujeruhiwa kwa tishu inazidi ile ya mwili kujihami na kuunga kwa jeraha.


Vile vile, kemikali za mwilini zinazotirishwa wakati wa majeraha yanapotokea zinaaminika chanzo na kuchochea majeraha ya kutumika sana kwa mwili.


Mwili huhitaji muda kidogo kukamilisha uponaji, endapo itatokea kujeruhiwa tena kabla ya kufanya hivyo ndipo ufanisi wa mwili kuponesha jeraha huvurugwa na kurudisha nyuma uponaji.


CHUKUA HII


Ni muhimu kwa wachezaji wanaotumika sana kupewa mapumziko au kuanzishwa kipindi cha pili au kutolewa mapema kipindi cha pili lengo ni kuwapa nafasi ya kupumzika ili kumlinda asipate majeraha.


Pamoja na kwamba hakuna namna wanatumika sana kote kote, katika klabu na mataifa yao lakini wapo ambao wana miili yenye ustahimilivu wa juu na hali ya kutumika sana.


Ndio maana pia haishangazi keshokutwa katika mashindano ya CAF au ligi kuu kama EPL kuwaona wachezaji wanaotumika sana wakicheza vizuri kama vile hawakuwa katika majukumu ya timu ya taifa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad