Hatma Ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ Na Yanga Kujulikana Leo Kwenye Ofisi Za TFF

 

fei Toto

ILE kesi kimkataba inayomuhusisha Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Yanga, inatarajiwa kutolewa ufafanuzi leo Alhamisi kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala jijini Dar es Salaam.


Hiyo ni baada ya Fei Toto kuomba ‘review’ juu ya majibu ambayo yalitolewa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.


Kamati hiyo ilitoa uamuzi juu ya shauri lililowasilishwa na Yanga baada ya Fei Toto kuvunja mkataba ikielezwa hakufuata utaratibu maalum, ambapo majibu yalitoka kwamba kiungo huyo bado ni mchezaji halali wa timu hiyo.


Taarifa zinabainisha kwamba, awali katika kesi hiyo, Fei Toto alikuwa anasimamiwa na wanasheria wawili, Makubi Kunju Makubi na Ndurumah Keya Majembe, lakini baadaye akaongezwa Fatma Karume ambaye ni mtoto wa rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na mjukuu wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.


Fatma Karume ambaye ni mwanasheria wa Kitanzania na wakili wa kujitegemea, mwanaharakati ambaye aliwahi kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), leo anatarajiwa kuliongoza jopo la mawakili wanaomsimamia Fei Toto katika kesi hiyo.


Yanga walifungua shauri hilo TFF wakipinga uamuzi wa Fei Toto kuvunja mkataba uliosalia mwaka mmoja na nusu na kurudisha kiasi cha shilingi milioni 112 ambacho alikitoa kwa ajili ya kutimiza takwa la kuvunja mkataba huo uliotarajiwa kumalizika Mei 30, 2024.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad