Hawa hapa waliojitosa kurithi mikoba ya Prof. Hosea TLS




Wakili Msomi Harold Sungusia
MAWAKILI wasomi watatu, Harold Sungusia, Reginald Shirima na Sweetbeert Nkuba, wamechukua fomu kuomba uteuzi wa kugombea nafasi ya urais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), katika uchaguzi mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Mei, 2023. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TLS hivi karibuni, mawakili hao ndio waliojitokeza kuchukua fomu za uteuzi hadi zoezi hilo lililoendeshwa na Kamati ya Uchaguzi ya chama hicho, lilipofungwa tarehe 3 Machi mwaka huu.

Mawakili hao wametia nia kutaka kugombea nafasi hiyo ambayo kwa sasa inashikiliwa na Prof. Edward Hoseah, anayemaliza muda wake.

Prof. Hoseah ameongoza taasisi hiyo kwa miaka miwili mfululizo kuanzia 2021 hadi 2023, ambapo kwa mujibu wa sheria za TLS haruhusiwi kugombea tena.


Taarifa hiyo inasema kuwa, watia nia hao wa kugombea Urais wa TLS, watafanyiwa mchujo na Kamati ya Uchaguzi ya TLS, kisha majina ya waliokidhi vigezo yatatangazwa.


Dk. Edward Hoseah, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)
“Kamati ya uchaguzi inawaalika wanachama kuwasilisha mapingamizi yoyote au taarifa kwa siri, kuhusu maadili ya watia nia pamoja na taarifa zozote zinazowahusu,” inasema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inasema kuwa, ratiba ya kampeni za uchaguzi huo itatolewa baada ya uteuzi wa wagombea kufanyika.


Miongoni mwa watia nia hao, Wakili Sungusia amejitosa kwa mara nyingine tena kuisaka nafasi hiyo, ambapo katika uchaguzi wa mwaka jana alishiriki na kuambulia nafasi ya pili.

Mbali na uchaguzi wa Rais, mawakili wanne wamejitosa kutia nia ya kugombea nafasi ya makamu wa Rais wa TLS, ambayo kwa sasa inashikiliwa na Wakili Gloria Kalabamu, anayemaliza muda wake.

Mawakili hao ni, Revocatus Kuuli, Emmanuel Augustino, Aisha Sinda na Fredrick Mtei.

Kwa upande wa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Vijana, wamejitokeza mawakili wawili kutia nia ya kugombea, ambao ni Edward Heche na Emmanuel Nyanza. Heche ametia nia kugombea mara ya pili ambapo kwa sasa anashililia wadhifa huo
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad