Tanzania imetajwa kuwa katika nafasi nzuri ya kuimarika katika sekta za uwekezaji, biashara na utalii kutokana na maridhiano ya kisiasa yanayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Wachambuzi wa masuala ya siasa walilieleza kuwa matunda ya maridhiano yameanza kuonekana kutokana na kitendo cha Rais Samia kualikwa na kuhudhuria kongamano la Baraza la Wanawake wa chama hicho (BAWACHA) kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Mtaalamu wa diplomasia na mchambuzi wa siasa nchini, Goodluck Ng’ingo alisema kitendo cha Rais Samia kuhudhuria kongamano hilo kinadhihirisha kuwa nchi ina amani, utulivu na maelewano.
“Miongoni mwa vitu vinavyovutia wawekezaji ni pamoja na sera za kudumu zisizobadilika pamoja na amani na utulivu wa kisiasa katika nchi.
“Kwa hali hiyo, ni dhahiri Tanzania inaenda kufaidika kama nchi kutokana na ongezeko la wawekezaji litakalotokana na utulivu na uhakika wa biashara,” aliongeza Ng’ingo.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Gabriel Mwang’onda alisema juhudi za Rais Samia za kujenga taifa lenye umoja, mshikamano na uzalendo zinajenga mazingira rafiki kwa biashara ya ndani na nje ya nchi hali itakayolifanya taifa kupata mapato zaidi.
Alisema kitendo cha Rais Samia kukubali kutengeneza taifa lisilo na mipasuko kinatuma ujumbe wa mshikamano na uzalendo.
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia na mchambuzi wa masuala ya siasa, Deus Kibamba alisema Rais Samia ameonesha ni nguli wa siasa.