Hoja ya Lema kuhusu bodaboda isigeuke kuwa malumbano kisiasa




UVUTAJI sigara ni tabia iliyojengeka miongoni mwa watu duniani na Tanzania haijaachwa katika hilo, ingawa pia ni tabia inayopigwa vita kuwa ina hasara kiafya.

Wataalamu wa tiba wanasema uvutaji sigara unaathiri afya ya mwili na kusababisha matatizo mengi, ikiwamo pia kupoteza maisha kutokana na kuathiriwa vibaya na sigara.

Imefika hatua kuwa mtu aliye jirani na mvutaji yuko katika hatari kubwa ya kuathiriwa na moshi wa sigara inayovutwa na mwingine, hivyo kutakiwa kujiepusha.

Pamoja na hali kuwa hivyo na sigara kupigwa vita kiasi hicho, lakini upande mwingine wa sarafu unaonyesha kuwa sigara ni biashara nzuri inayotoa mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi.

Ndiyo sababu kuna viwanda vya sigara, pia kuna wakulima wa tumbaku, ambayo ni malighafi ya sigara na wamekuwa wakisaidiwa kwa mbolea na pembejeo zingine, ili kuzalisha kwa wingi na kulisha viwanda.


Hivyo sigara ni hatari kwa maisha ya binadamu, ina faida pia kwa maisha yao, kupitia viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo na kutoa ajira, vilevile kuchangia pato la taifa.

Kama tunakubaliana katika hili, basi tutafakari pia katika kauli ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Lema aliyekuwa uhamishoni nchini Canada kisiasa, alirejea hivi karibuni nchini na kupokewa na umati wa wafuasi wa chama chake, wakiwamo madereva wa bodaboda katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wakafuatana mpaka jijini Arusha.


Wakati wote wakifurahia mapokezi hayo, kumbe yeye moyoni alikuwa akisononeka, kuwaona wafuasi wake watumia bodaboda wakiteseka, licha ya wao kufurahia ujio wa kiongozi wao. Hakuzuia hisia zake, akasema:

“Bodaboda, wakati ninyi mnanipokea kwa shangwe, mimi nilikuwa na huzunika. Bodaboda si a ira, ni umasikin iunaopitiliza. Hiyo ni ajira ya laana, ikemeeni. Hamuwezi kufanya ajira kwa kukimbiza upepo. Sh 7,000 kwa siku! Hapana!”

Alipoisikia kauli hiyo, Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu wa  Chama Cha Mapinduzi (CCM), akaibuka na kumpinga Lema kwa maneno yake akifafanua kuhusu bodaboda.

Akasema: “Kuna nchi nyingi zinaongoza kwa kuwa na waendesha bodaboda. Hii ni kazi ya heshima na inarahisisha usafiri wa watu kujenga uchumi wa nchi.


“Kitendo cha mwanasiasa huyo kuwatukana bodaboda katika taifa letu kwamba wamelaaniwa, hatuwezi kuacha bila ya kujibiwa kwenye majukwaa ya kisiasa.”

Akasema kuwa CCM inawaheshimu na itawasaidia kwa kuanzisha mikakati ya kuchochea maendeleo yao kiuchumi.

Hizo ndizo siasa za  nchini. Tayari suala muhimu na nyeti kama hilo limehamia kwenye majukwaa, badala ya kutafakari hoja kwa uzito wake.

Ili kuongeza uzito wa hoja yake, Lema alipomsikia, Kingu akaona aje na lingine akiwaambia, bodaboda hawana bima kama ilivyo kwa magari, hivyo wapatapo ajali hawalipwi chochote zaidi ya kuishia kupata ulemavu wa kudumu.

Nadhani Lema hakuwa na nia ya kuwatukana, kama inavyoonekana, lakini alikuwa akihadharisha kutoka na na madhila wanayoyapata vijana hao yakiwamo ya magonjwa yatokanayo na upepo na baridi kama vile baridi yabisi.

Madhila kama ya ajali, katika hospitali nyingi hivi sasa kuna wodi maalumu za madereva hao ambao kila siku wanapata ajali barabarani na kuishia kupoteza maisha au kukatwa baadhi ya viungo.

Ninavyohisi Lema katamka kwa kuwapenda vijana wake na ndiyo sababu akaamua kufunguka kuwatetea kwa njia hiyo. Hakuna asiyewatambua kuwa ni Watazania wanaojitafutia. Hata Rais Samia Suluhu Hassan amelisema hilo hadharani.

 Maoni yangu mojawapo, kurahisisha huduma hizo za usafiri, bora kuhalalisha za miguu mitatu kuliko miwili, ikishindikana tuhakikishe wana bima, lakini pia wanasimamiwa kuheshimu sheria za barabarani na si kuwadekeza kwa kuwapunguzia faini ili waendelee kuvunja sheria.

Inafaa tukapunguze siasa kwenye maswali magumu. Alamsiki!




Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad