JICHO LA MWEWE: Kituo gani kinafuata kwa Fei Toto?




ALIPOOMBA au tuseme walipoomba marejeo kuhusu kesi yake ya kujaribu kuvunja mkataba, upande wa Feisal Salum ‘Fei Toto’ umepigwa chini tena. Inaonekana kwamba uamuzi wa awali wa kamati iliyokaa kujadili kesi yake umebakia vile vile kwamba Fei ni mchezaji wa Yanga.

Nini kinafuata kwa Fei Toto? Ni swali gumu kidogo. Ni wazi kwamba kichwa cha Fei kimebadilika na haitaki tena Yanga. Lakini kinachoonekana zaidi ni kwamba upande wake pia umebadilika kabisa na hauitaki tena Yanga.

Siku moja kabla ya hukumu Mama yake alirekodiwa na kuongea maneno mengi ambayo hayakuwa na maana. Sihitaji kurudia alichoongea lakini ni wazi kwamba hakikuwa na maana kwa sababu kwanza mama haelewi sana masuala ya mpira lakini pia haelewi masuala ya mikataba.

Akatushangaza kutuambia kwamba Feisal alikuwa anateseka Yanga. Yanga ipi? Hii ambayo alikuja kusaini mkataba mwingine au ile ya kina Mwinyi Zahera? Nadhani alikuwa anazungumzia Yanga hii ambayo inamlipa mwanae mshahara wa shilingi milioni nne kwa mwezi.


Kufikia hapo ni wazi kwamba Fei amevunja daraja la uhusiano na Yanga, lakini zaidi hata mama yake mzazi amevunja daraja la uhusiano na Yanga. Ni mama ndiye ambaye wiki iliyopit alitupa kioja cha ajabu kiasi cha watu kuanza kula ugali na sukari mitaani.

Na sasa nini kinafuata kwa Fei? Hatujui. Tunaweza tu kubashiri kwamba leo Jumatatu kila upande utaelezwa sababu za uamuzi wa kamati na baada ya hapo kina Fei wanaweza kwenda CAS kudai haki yao zaidi. sijui itachukua muda gani.

Kitu ambacho kinaonekana ni kwamba kuna watu wapo nyuma ya Fei na wanaonekana kumpoteza. Kwanza kabisa haya yote ambayo yanatokea hayakupaswa kutokea sasa hivi. Washauri wake walimshauri vibaya.


Fei hakupaswa kuanzisha timbwili hili sasa hivi. Alipawa kusubiri mpaka mwisho wa msimu kuanzisha alichoanzisha. Alipaswa kuendelea kucheza soka huku akisubiri ushauri wa namna ya kufanya pindi msimu utakapofika mwisho.

Ingawa bado ingekuwa ngumu kuvunja mkataba na watu wa Yanga lakini walau kungekuwa na nafasi ya yeye na watu wake kutafakari zaidi kila kinachotokea na mchezo wenyewe wa soka ungekuwa katika mapumziko.

Lakini kinachotokea sasa hivi ni kwamba Feisal hachezi soka. Anafanya mazoezi nyumbani wakati wenzake wapo katika viwanja mbalimbali vya soka ulimwenguni. Sidhani kama anajisikia raha sana. Anakaa katika televisheni yake wikiendi hii ameangalia Liverpool na Manchester United, kesho anatazama Simba dhidi ya Vipers keshokutwa anawatazama wachezaji wenzake wa Yanga wakicheza na Real Bamako. Haivutii.

Kama si kusubiri mwisho wa msimu basi Fei angekuwa na washauri wazuri sana angesubiri mpaka mwisho wa mkataba wake na kuwa mchezaji huru. Jaribu kuangalia, labda Fei alishawishika kwamba mkataba wake umebakia muda mrefu lakini leo ni Machi na bado miezi miwili tu msimu uishe.


Msimu ujao ungekuwa mfupi zaidi kwake na kwa Yanga. Msimu wa soka una miezi kama tisa tu. ambacho Fei alipaswa kufanya ni kutosaini mkataba mpya Yanga. Angekuwa anacheza, anajituma, anaongeza thamani yake. Mwisho wa msimu ujao timu tatu zingeingia vitani. Yanga, Simba na Azam.

Clatous Chama kwanini analipwa pesa nyingi Simba? Kwanini alipata pesa ndefu ya kusaini mkataba mpya kabla hajaenda Morocco? Ni kwa sababu alijaribu kutiririsha mkataba wake mpaka mwishoni mwa msimu. Yanga waliingia vitani, Simba wakapagawa. Chama alisaini mkataba wake mpya Machi. Miezi miwili kabla ya kumalizika kwa mkataba wake.

Fei angejituma na kukaa kimya tu. Mei 2024 ingefika kwa urahisi tu kwake na angekuwa mchezaji huru. Kama kuna timu inamshawishi sasa hivi basi ingeweza kumlipa pesa nyingi zaidi kuliko ilivyoahidi kumlipa sasa hivi. Vita ingekuwa kubwa ya kuwania saini yake na thamani yake ingekwenda juu zaidi.

Tatizo kubwa ni ‘timing’ yake katika kuvunja mkataba. Ambacho nafahamu ni kwamba wachezaji wetu wazawa wameanza kushawishiwa kwamba wanastahili kulipwa pesa kubwa kama ilivyo kwa kina Aziz Ki au Chama.


Ambacho hatujui ni kwamba chukua mfano wa Aziz Ki. Alitua Yanga akiwa mchezaji mwenye sifa lukuki. Anachezea timu ya taifa ya Burkina Faso, lakini pia alikuwa amesajiliwa akiwa mchezaji bora katika Ligi Kuu ya Ivory Coast. Fei wakati anasaini mkataba wake wa kwanza na kisha wa pili akiwa na Yanga hakuwa na wasifu huu.

Fiston Mayele alichukuliwa na Yanga kutokea AS Vita. Alikuwa anashika nafasi ya pili kwa ufungaji wa mabao Ligi Kuu ya Congo lakini pia alikuwa ameifikisha Vita katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa. Wakati Fei anasaini mikataba miwili na Yanga hakuwa na wasifu huu.

Kitu kizuri ni kwamba licha ya kuletewa wachezaji wenye wasifu mkubwa lakini Fei kwa sasa amejitengenezea wasifu huo. Ameipa Yanga ubingwa, amefunga mabao muhimu, ameipeleka Yanga katika makundi ya Shirikisho. Kuanzia hapo angekaa mezani na kuomba alipwe kama kina Mayele katika mkataba wake unaofuata.

Tatizo washauri wake hawakuzingatia haya badala yake wakaangalia hali ilivyo sasa tofauti na namna yeye na wenzake walivyoingia katika timu. Ni kama leo Clement Mzize atake kulipwa kama Kenneth Musonda kwa sababu tu hapa karibuni amefunga mabao mengi kuliko Musonda.

Nini kinafuata kwa Fei? Sifahamu vema. Kama ningepewa nafasi ya kumshauri Fei ningemwambia arudi kucheza Yanga lakini asisaini mkataba mpya mpaka mwisho wa mkataba wake. ingemfanya aendelee kuwa fiti uwanjani.


Walio nyuma yake wanaweza kumshauri kwamba asirudi na akae nje mpaka mkataba wake umalizike Yanga lakini ukweli ni kwamba kama Fei hatacheza mpira wa ushindani kwa mwaka na nusu basi anaweza kurudi uwanjani akiwa ovyo. Nyakati huwa hazimsubiri mtu.

Lakini kwa upande mwingine kama ningekuwa mshauri wa Yanga ningeamua tu kuziita mezani timu ambazo zinamtaka Fei na kumpiga bei. Yanga ni kubwa kuliko Fei. Ni kubwa kama taasisi lakini ni kubwa kwa umri pia. Kuna mastaa wengi wamepita Yanga na bado Yanga imeendelea kuwa imara.

Kwa kukumbusha tu, mwaka 1975 Yanga waliwahi kufukuza timu nzima klabuni lakini leo wameendelea kuwa miongoni mwa timu imara nchini. Kwanini wahangaishwe na Fei mmoja tu?




Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad