"NI maamuzi magumu, ila imebidi iwe hivyo, kwani muda muafaka ndiyo umewadia, sijali wangapi watalia, lakini ni lazima maisha ya siasa yaendelee hata kupitia vyama vingine, si lazima kufanyia ndani ya CUF tu".
Hivyo ndivyo mwanasiasa machachari Abdul Kambaya, ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi, katika Chama cha Wananchi (CUF), kabla ya yeye na wenzake kutimuliwa mwanzoni mwa mwaka 2021.
Akizungumza na gazeti hili jijijini Dar es Salaam, Kambaya ambaye sasa amejiunga na CHADEMA, anasema ameachana na kesi aliyofikisha katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, akipinga kuvuliwa uanachama wa CUF na sasa anasonga mbele.
"Kesi inakaa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa zaidi ya mwaka mmoja bila kutolewa uamuzi, nimeona isiwe shida , niachane nayo na nijiunge na chama kingine niendelee na harakati zangu za kisiasa," anasema Kambaya.
Mwanasiasa huyo aliyejiunga na CHADEMA hivi karibuni Machi 11, anasema wapenda haki wenzake waliokuwa wanachama wa CUF 400 mkoani Dar es Salaam wameungana naye katika uamuzi huo.
Anadai wanachama hao wamemfuata CHADEMA licha ya kwamba , haijathibitika rasmi uwapo wa takwimu hizo kutoka uongozi wa chama hicho.
"Muafaka ndiyo umewadia, sijali wangapi watalia, lakini ni lazima maisha ya siasa yaendelee kupitia huku niliko sasa, lakini ofisi ya Msajili ijue kumkumbatia Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahimu Lipumba, si kukisaidia ni kukiua," anasema.
Katika ufafanuzi wake anasema, ruhusa ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa imeonyesha jinsi ambavyo wanachama wa CUF wasiopenda dhuluma wamekikimbia na kujiunga na vyama vingine.
"Hivi karibuni tulishuhudia wanachama wa CUF mkoani Dar es Salaam wakijiunga na vyama vingine. Hizo ni salamu kwa Msajili kuwa, kumkumbatia Mwenyekiti Lipumba siyo kusaidia, bali kuondoa CUF kwenye ramani ya siasa na dunia," anasema.
HAKIFI KITU
Wakati Kambaya akikitabiria chama hicho kifo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bara, Magdalema Sakaya, anasema chama hakitakufa, kwa kuwa kimejengwa katika misingi imara isiyoyumba.
"Kwanza Kambaya si mwanachama wa CUF, hivyo si sahihi kuzungumzia sana, aiache CUF tena asitegemee kwamba chama kitakufa, imejengwa kwenye ngome madhubuti. Hata mimi nikiondoka siwezi kusababisha ikafa," anasema Magdalena bila kueleza uimara wa ngome ya chama chao ni nini.
Aidha, anasema wapo wanachama wengi ambao wamekuwa viongozi wa serikali ambao walikikimbia na kukiacha kikiwa imara, huku akimtaka Kambaya aendelee na siasa huko aliko, si kuzungumzia CUF.
Naibu Katibu Mkuu huyo anasema kauli ya Kambaya haiwezi kuyumbisaha wanachama wa CUF kwa mambo yasiyokuwa na msingi na kwamba badala yake wataendelea kuungana katika kukiimarisha chama hicho."Chama hiki kiko imara na kitaendelea kuimarika kutokana na uwezo wa viongozi wake ambao wamepata sifa kutokana na umahiri wao wa masuala ya uchumi na siasa," anaeleza.
Anasema chama hicho siku zote kimekuwa mstari wa mbele, katika kusimamia misingi ya haki na usawa kwa wote na kwamba kitaendelea kufanya hivyo kwa wanachama wake na wapenzi wa CUF.
KIGUGUMIZI MSAJILI
Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, anapoulizwa kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwake, kuhusu kumkumbatia, Profesa Lipumba, anasema kwa kifupi kuwa 'no comments'."Huyo mtu wako si kashahamia CHADEMA? Mambo ya CUF awaachie wenyewe. Kakwambia kwamba Jaji kukumbatia migogoro siyo kumsaidia Lipumba, nasema no comment,"
Mwaka 2021, CUF ilitangaza kuwavua uanachama viongozi wake saba, wakiwamo 14 waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali kama madai ya kula njama za kukihujumu chama hicho.
Baadhi yao walikuwa ni Mjumbe wa Baraza Kuu, Abdul Kambaya, mjumbe mwenzake Hamis Mohamed Faki, aliyekuwa mbunge wa Mchinga mkoani Lindi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa chama hicho, Hamidu Bobali.
Mbali na hao, wengine waliofukuzwa ni Hamida Abdallah Huweishi, mgombea mwenza wa Profesa Lipumba katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Chande Naibu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana ya CUF (JUVICUF).Katika kundi hilo, walikuwamo pia Ali Makame Issa, Mtumwa Ambari Abdallah , Mohamed Vuai Makame na Dhifaa Bakari ambao wote nao walikuwa ni wajumbe wa Baraza Kuu la CUF.
Kitendo hicho cha kufukuzwa kiliwafanya wabishe hodi katika ofisi za Msajili wa Vyama vya Siasa, jijini Dodoma Desemba 2021, ili kusaka haki yao, lakini Kambaya anadai kuwa hadi sasa ofisi hiyo imekuwa kimya.Kwa uamuzi huo wa Kambaya, ni wazi sasa sintofahamu hiyo ya waliokuwa wanachama wa CUF inaweza kuwa imeshia hapo, baada ya kinara wao kubwaga manyanga na kujiunga na CHADEMA.