MABEKI wa Simba, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein 'Tshabalala' wameongezwa katika kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' kinachojiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za Mataifa Afrika (AFCON) dhidi ya Uganda.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) , Wallace Karia amesema kuitwa kwa nyota hao ni pendekezo la Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Adel Amrouche.
"Maneno yalikuwa mengi sana baada ya uteuzi uliofanyika mwanzoni lakini tumeona matunda yake, kuongezwa kwa Kapombe na 'Tshabalala' ni pendekezo la Kocha Mkuu, Adel Amroache na tayari wamejiunga kambini na wenzao."
Aidha Karia amesema wao kama TFF hawajakaa wala kumshauri Amrouche kuhusu uteuzi wa kikosi isipokuwa walimpa uhuru wakiamini ni kocha mzuri na anayetambua vyema wachezaji kwani alishaanza kuwafuatilia kitambo.
"Sisi hatuwezi kuingilia majukumu yake kwa sababu tunaamini katika weledi aliokuwa nao, jukumu kubwa kwetu ni kuendelea kumpa ushirikiano ili kwa pamoja tufikie malengo yetu kama taifa," amesema Karia.
Stars itashuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumanne hii ya Machi 28 ikiwa na morali kubwa baada ya mchezo uliopita kushinda bao 1-0 lililofungwa na, Simon Msuva katika mechi iliyopigwa nchini Ismailia Misri.
Katika kundi F Stars iko nfasi ya pili ikiwa na pointi nne nyuma ya vinara Algeria yenye pointi tisa baada ya kushinda michezo yote mitatu.
Niger ni ya tatu na pointi mbili huku Uganda ikiburuza mkiani baada ya kukusanya pointi moja.