Kocha Mkongo aivusha Yanga nusu fainali CAF, awataja Mayele, Musonda



KWA sasa ukimgusa shabiki yeyote wa Yanga tu atakwambia kwa jeuri niache, hii ni kutokana na chama lao kuongoza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu Bara kwa mpigo, lakini sasa wameongezewa mzuka baada ya kocha mmoja Mkongomani kuitabiria kwenda nusu fainali.
Yanga ni moja kati ya timu zilizofuzu robo fainali ya michuano ya CAF ikitokea Kundi D licha ya kuwa na mchezo mmoja mkononi na sasa inajiandaa kwenda kukamilisha ratiba kuvaana na Monastir ya Tunisia waliofuzu pamoja katika kundi hilo.
Lakini wakati wakifurahia kutinga hatua hiyo ikiwa ni rekodi kwa Yanga tangu iliposhiriki hatua ya makundi ya michuano ya CAF kuongoza msimamo na kuvuka kwenda hatua ya juu, kocha aliyewahi kuinoa na mwenye rekodi zake Afrika, Raoul Shungu ameitabiria kufika mbali zaidi na hatua hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti kutoka DR Congo, Shungu aliyeinoa Yanga iliposhiriki makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza 1998, alisema kwa mziki aliouona kwa timu hiyo anaiona sio kufika robo fainali, bali inaweza kabisa kwenda nusu fainali.
Shungu alisema kinachoipa jeuri Yanga ni ubora wa soka inalocheza kwa sasa ikiwa na mbinu za kisasa zaidi zikionyesha na kusema kocha wa sasa wa timu hiyo, Nasreddine Nabi amethibitisha ubora wake kwa jinsi alivyotengeneza timu imara uwanjani.
Kocha huyo alisema, safu ya ushambuliaji ya Yanga inayoongozwa na mshambuliaji na winga aliyowahi kuwanoa wakiwa AS Vita, Fiston Mayele, Jesus Moloko na Mzambia Kennedy Musonda inafanya kazi bora na kuibeba timu hiyo kwa sasa.
"Namuona Fiston (Mayele) ameendelea kuwa bora, lakini Jesus (Moloko) yuko katika kiwango bora sana, nilisema tangu mapema wakati wanakuja huko hao watu wataipa nguvu kubwa Yanga ,lakini nimemuona na yule mshambuliaji wa Zambia (Musonda) hawa kwa pamoja wanaifanya safu ya ushambuliaji ya Yanga kuwa na nguvu kubwa," alisema Shungu anayeingoa Vita na kuongeza; "Ni mara chache timu imebahatika kuwa na watu bora wa namna hiyo, hapa sasa Vita ndio tunaunda timu sio kazi rahisi kuwa ubora kama huo ambao unauona Yanga inahitaji muda.
"Nawafuatilia sana Yanga, hivi karibuni niliangalia mechi yao na TP Mazembe hata ile waliyocheza na timu ya Tunisia (Monastir) hapo Tanzania pia nimeiona, wanacheza vizuri, wanashinda kwa ubora wa mbinu za uwanjani hii ni nzuri sana, wana timu bora ambayo inaweza kufika mbali hata zaidi ya nusu fainali."
Kuhusu kocha wa Yanga, Shungu alisema; "Kocha wao anaonekana amefanikiwa mtaji mzuri kwake ana wachezaji bora, lakini lazima tuheshimu kazi nzuri yake kwa jinsi alivyoiunganisha timu na kucheza kisasa sana."
Shungu ambaye ni kocha mkuu wa AS Vita kwa sasa alisema, Yanga kuanzia hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika hawatakuwa wachanga kwa kuwa ndani ya kikosi chao wana wachezaji wazoefu ambao wamecheza zaidi ya hatua hiyo, huku akiwataja mastaa wengine wanaoibeba.
Aliwataja mastaa kama Joyce Lomalisa aliyecheza Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na AS Vita na kuchukua taji hilo 2014,a mabeki Yannick Bangala, Djuma Shaban na Moloko waliocheza fainali ya Shirikisho 2018 na kupoteza huku winga Tuisila Kisinda aliyechukua taji la Shirikisho Afrika msimu wa 2022 akiwa na RS Berkane watakuwa wenyeji wa hatua hizo ngumu kwa wenzao.
Yanga inatarajiwa kusafiri Alhamisi ijayo kwenda DR Congo kuvaana na TP Mazembe kwenye mechi ya kukamilisha ratiba itakayopigwa Aprili 2 jijini Lubumbashi na iwapo itashinda itamaliza kama kinara wa kundi na kukwepa kukutana na vigogo waliopo kwenye michuano hiyo ya Shirikisho
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad