BOSI wa Manchester United, Erik ten Hag, amesema ni aibu kubwa hasa kwa wachezaji wake kuonesha kiwango duni ndani ya Anfield na kupelekea kupokea kipigo cha nguvu.
Hii ni baada ya Manchester United kuchakazwa kwa mabao 7-0 na Liverpool katika mchezo wa Premier uliochezwa juzi Jumapili.
Man United msimu huu ina rekodi ya kupokea vipigo vikubwa ambapo kabla ya kufungwa 7-0, ilifungwa 6-3 dhidi ya Manchester City.
Ten Hag alisema: “Ilikuwa mbaya. Lakini ilikuwa mbaya zaidi kwa mwaka huu kutokana na kiwango kibovu ambacho walionesha wachezaji wangu.
“Tulipoteza mchezo kipindi cha kwanza, ila kipindi cha pili ilibidi kubadilika, lakini haikuwa hivyo, wakazidi kuongeza mabao.
“Walichoonesha wachezaji wangu hakikuwa profesheno, walitakiwa kuonyesha kazi yao, ila wakashindwa.
“Najua mashabiki hawakupenda kile ambacho tulionesha ndiyo maana wakawa na uwezo wa kutoka uwanjani mapema kwa sababu tumetia aibu mbele yao.
“Kwa kilichotokea ni kibaya, kimenikera na kutia hasira, hakikubaliki hata kidogo kwetu, kile ambacho kilikuwa kinaonekana uwanjani kilikuwa hakieleweki, kila mchezaji alicheza kwa namna yake na sio kama timu, nimekasirishwa kwa kilichotokea.
“Hata katika vyumba vya kubadilishia nguo nimewaeleza wazi kuwa kilichotokea hakikubaliki hata kidogo kwani walifanya maamuzi kadhaa ambayo hayakuwa sahihi kwa timu.
“Lakini hii ni mechi moja ambayo tumepoteza kwa sasa, wachezaji wanatakiwa waangalie wapi walikosea, ninaamini timu yangu itasimama na kuwa imara tena kuona kila kitu kinaenda sawa.”