Wiki hii Tanzania imetoa misaada kwa mataifa mawili ya Uturuki na Malawi yaliyopitia masaibu na kuathiri maelfu kwa maelfu ya watu.
Tanzania imeisaidia Malawi msaada wenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 ukiwa kwenye mfumo wa fedha taslimu na mahitaji ya kibinadau, kufuatia nchi hiyo kukumbwa na kimbunga cha tropiki cha Freddy.
Magari 37 Makubwa yalipelekwa Malwi kusambaza misaada ya kibinadamu, mahema, chakula, mablanketi 6,000. Ikatoa msada wa kijeshi wa nguvu kazi na helkopta mbili kwa ajili ya kusaidia huduma za uokoaji na usambazaji wa misaada ya kibinadamu.
Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania ndilo lilipeleka misaada hiyo na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Humphrey Polepole aliongoza makabidhiano.
Kama haitoshi nchi hiyo pia imetoa msaada wa Dola za Marekani 1,000,000 kwa Uturuki kufuatia madhara ambayo nchi hiyo inepata kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea mwezi Februari mwaka huu. Kwanini kuna mijadala kwa hatua hiii ya Tanzania kutoa misaada?
Kwanini Tanzania itoe misaada ilhali yenyewe inahitaji misaada?
Msaada
Chanzo cha picha, G/Msigwa
Hili ni swali ambalo linajenga mjadala hasa kwenye mitandao ya kijami. Kwanini Tanzania itoe misaada wakati yenyewe inahitaji msaada, wate wake wanahitaji msaada na inaonekana haijajitosheleza?
Kiuchumi, ni miongoni mwa nchi masikini duniani. Mamilioni ya watu wanasotea huduma za afya, upungufu wa wataalamu wa afya, dawa, vifaa tiba, mamilioni hawafikiwi na elimu bora huku kukiwa na upungufu wa madawati, walimu, na miundo mindu bora ya elimu.
Pengine bilioni tatu za misaada ilizotoa katika juma moja lililopita zingeweza kujenga makumi ya madarasa, ama kununua vifaa tiba ama kujenga zahanati na kuokoa maisha ya maelfu ya watu.
Mamilioni ya watu hawana ajira, uduni wa teknolojia, huku mamia ya watoto chini ya miaka 5 maisha wakipoteza maisha kwa udumavu wengine kwa kukosa huduma bora za afya. Matatizo ni mengi lakini bado imekwenda kutoa misaada nje.
Chanzo cha picha, W/afya
Msaada
Maelezo ya picha, Tanzania ikipokea misaada kutoka Misri
‘Ni utamaduni wa kiutu na kibinadamu, ni urafiki na undugu, si rahisi kuona ndugu yako ama binadamu mwenzako anaathirika, amepata majanga makubwa, ukashindwa kumsaidia, watanzania hatujaumbwa hivyo’, anasema Raphael Magoha, mtaalamu wa fedha anayefuatilia masuala ya kijami.
Lakini hoja hii ya Magoha, haonekani kukubalika na baadhi.
‘Kila siku tunapokea misaada, mwaka jana tu tumepokea madawa toka Misri, inaonyesha tunauhitaji lakini na siÄ™ tunatoa msaada kwa wengine, inachanganya’, anasema Seif Shangali.
Anachokisema Shangali pengine anarejea msaada vifaa tiba uliotolewa Septemba, 2022 na Misri kwa Serikali ya Tanzania, kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini humo. Vifaa hivyo vilikuwa na vyenye thamani ya dola za Kimarekeni elfu 27 (USD 27,000), ambazo ni sawa na takribani shilingi milioni 62.9 za kitanzania.
Si jambo geni Lakini kwa nini sasa?
Chanzo cha picha, Getty Images
Ukombozi
Maelezo ya picha, Tanzania wakati wa utawala wa Nyerere ilishiriki si mara moja kusaidia ukombozi wa mataifa mengi Afrika
Miaka minne iliyopita, chini ya utawala wa Rais John Pombe Magufuli, Tanzania pia ilizisaidia chakula na wa nchi za Malawi, Zimbabwe na Msumbiji zilizokuwa zimekumbwa na kimbunga na mafuriko. Ilitoa tani 8 za dawa kwa kila nchi, na tani 214 za chakula.
Profesa Paramagamba Kabudi, aliyekuwa waziri wa masuala ya kigerni na waziri wa afya Ummy Mwalimu ndiye waliokabidhi misaada hiyo kwa mabalozi wa nchi hizo nchini Tanzania, na Kabudi alisikika akisema hatua hiyo ni ‘‘Kuendeleza urafiki mwema na utamaduni wa kusaidiana’’.
Hakuna asiyefahamu Tanzania ilivyokuwa kitovu cha ukombozi wa nchi nyingi za Afrika. Ulikuwa msaada mkubwa zaidi wa kukomboa mataifa ya Afrika yaliyokuwa yanapambania uhuru. Rais wa kwanza Julius Nyerere aliungana na viongozi wengine mashuhuru Afrika kama Nelson Mandela, Samora Machel, Joaquim Chissano na Kenneth Kaunda kusaidia nchi zote za Kusini mwa Afrika kujipatia uhuru wake wa bendera.
Tanzania pia ilikuwa mwenyeji wa vikundi vingi vya wapigania uhuru na kutoa hifadhi achilia mbali kuwa Makao ya Kamati ya Ukombozi ya Bara la Afrika.
Lakini kwanini sasa? Pengine ni kutokana na athari mbaya zaidi zilizojitokeza kwa mataifa iliyoyasaidia. Malawi imekumbwa na kimbunga cha Freddy kilichosababisha vifo vya zaidi ya watu 300 katika nchi hiyo na Msumbiji.
Mwanzoni mwa mwezi Februari, 2023, Uturuki ilikumbwa na moja ya majanga makubwa zaidi duniani lililopoteza zaidi ya watu 45,000 kati ya watu zaidi ya 50,000 waliofariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo na Syria.
Maelfu ya watu wamekuwa mahitaji ya kibinadamu kama chakula, dawa na malazi. Umoja wa Mataifa kupitia mfuko wake Mkuu wa dharura (CERF) ulitenga zaidi ya dola 25 milioni kwa ajili ya kusaidia watu walioathirika na tetemeko hilo.
‘Mataifa mengi, mashirika mengi yalijitolea kusaidia, kwanini isiwe Tanzania hata kwa kidogo tu?, hiyo inaonyesha mshikamano na kuguswa, kuna kesho na keshokutwa’, alisema Magoha