Mamia ya watu wameandamana nchini Ugiriki baada ya treni iliyokuwa imebeba abiria takribani 350 kugongana uso kwa uso na treni ya mizigo na kusababisha vifo vya watu 46 na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Waandamanaji hao walikabiliana na polisi nje ya makao makuu ya Hellenic Train mjini Athens – kampuni inayohusika na utengenezaji wa miundombinu ya reli nchini Ugiriki.
Maandamano pia yalifanyika Thessaloniki na mji wa Larissa, karibu na mahali ambapo maafa yalitokea Jumanne usiku huku Serikali ikisema kuwa uchunguzi wa huru utatoa maelezo kamili.
Siku tatu za maombolezo ya kitaifa zimetangazwa kote nchini kufuatia kisa hicho, ambapo treini ya abiria iligongana na treni ya mizigo na kusababisha mabehewa ya mbele kuwaka moto.
Kwa mujibu wa taarifa ya vyombo vya habari vya Ugiriki vinasema kuwa wengi waliokuwemo ndani ya treni hiyo walikuwa wanafunzi wenye umri wa miaka 20 waliokuwa wakirejea Thessaloniki baada ya wikendi ndefu kusherehekea Kwaresima ya Orthodox ya Ugiriki.
Waziri Mkuu Kyriakos Mitsotakis alisema makosa mabaya ya kibinadamu ndio yalisababisha maafa hayo.
Msimamizi wa kituo cha Larissa mwenye umri wa miaka 59 amefunguliwa mashtaka ya kuua bila kukusudia, ambapo amekana kosa lolote, akilaumu ajali hiyo kwa hitilafu ya kiufundi.