Dar es Salaam. Hivi unakumbuka mara ya mwisho uliumwa maradhi gani?
Ripoti ya utafiti wa ufuatiliaji kaya (NPS) 2020/2021, imeyaorodhesha maradhi matano yanayoongoza kulaza wagonjwa hospitalini nchini, ambayo ni malaria (asilimia 0.7), matatizo ya uzazi (asilimia moja), homa (asilimia 0.4), tumbo (asilimia 0.6), mapafu (asilimia 0.2) na magonjwa mengine (0.9)
Utafiti huo uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar (OCGS) ulihusisha kaya 3,352 kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
Hata hivyo, kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya 2022/2023, magonjwa yasiyoambukiza katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, yaliongoza kulaza wagonjwa hospitali.
“Wagonjwa walio zaidi ya umri wa miaka mitano, walilazwa kwa sababu ya malaria (wagonjwa 76,834), kichomi (wagonjwa 65,904), magonjwa ya mfumo wa mkojo (wagonjwa 50,723), upungufu wa damu (wagonjwa 45,997) na shinikizo la juu la moyo (wagonjwa 43,974),”ilionyesha sehemu ya hotuba hiyo.
Magonjwa yaliyoongoza kwa wagonjwa kulazwa (IPD) kwa wenye umri chini ya miaka mitano yalikuwa ni kichomi, malaria na kuharisha.
Malaria kinara
Ripoti zote mbili za NBS na hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya zimeitaja malaria kuwa ni moja ya magonjwa yanaoongoza kulaza watu, huku wataalamu wa afya katika vituo mbalimbali vya afya wakikazia juu ya uwepo wa ugonjwa huo.
Kama hiyo haitoshi, wakati ugonjwa huo ukiwa unapuuzwa na watu wengi kwa sasa, Shirika la Afya Duniani (WHO), limeitaja Tanzania miongoni mwa nchi 17 zenye viwango vya juu vya maambukizi ya malaria duniani.
Vilevile, ripoti iliyotolewa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), inaonyesha zaidi ya watu milioni 45 nchini Tanzania wako katika hatari ya kuugua malaria, kwa sababu ya hali ya hewa na topografia, hii ni sawa na kusema watu 7 kati ya 10 nchini wapo hatarini kuugua ugonjwa huo.
Oktoba 20,2022, akizindua akizindua mradi mpya wa kutokomeza malaria ujulikanao kama ‘Shinda malaria, dhibiti malaria’ jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema bado kuna mzigo mkubwa wa wagonjwa wa malaria ikilinganishwa na idadi ya watoa huduma.
“Watu 10 kati ya 100 wanakwenda vituo vya afya kwa sababu ya malaria, bado mzigo ni mkubwa, watumishi wa afya ni wachache,” alisema Ummy.
Huku wataalamu wa afya wakiitaja kinga kubwa ya ugonjwa huo ni matumizi ya chandarua kilichowekwa dawa ya mbu, takwimu za ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS/MIS-2021/2022), zinaonyesha idadi ya watu wanaotumia vyandarua nchini imepungua kwa asilimia nne.
“Watanzania waliotumia vyandarua vyenye dawa mwaka 2022 walikuwa asilimia 74 ikilinganishwa na Watanzania asilimia 78 waliotumia mwaka 2017,”alisema.
Aidha, ripoti hiyo iliyozinduliwa mapema mwaka huu imeonyesha maambukizi ya malaria kwa watoto chini ya miaka mitano yameongezeka nchini.
“Watoto wenye malaria wameongezeka kutoka asilimia saba mwaka 2017 hadi asilimia nane mwaka 2022,”ilisema ripoti hiyo.
Mikoa inayoongoza kwa maambukizi ya malaria kwa watoto ni Tabora (asilimia 23), Mtwara (asilimia 20) na Kagera (asilimia 18).
Akizungumzia ugonjwa huo, Mwanahawa Hija, Mkazi wa Mabibo Farasi jijini hapa alisema “Mtoto wangu kwa mwaka jana aliumwa mara mbili tatizo likiwa ni malaria na alilazwa Hospitali ya Amana,”alisema
Alipoulizwa kuhusu matumizi ya chandarua alisema: “Kwa sasa mimi situmii ila napulizia dawa ya mbu na nahakikisha milango na madirisha muda wote vimefungwa ili wasiingie ndani,” alisema.
Ripoti ya NPS imeonyesha wagonjwa wengi wanaolazwa hospitalini na kusumbuliwa na maradhi mara kwa mara ni wenye umri wa zaidi ya miaka 60, wakifuatiwa na wenye miaka 25 hadi 34.
Kwa upande wake, Dk Alex Makalla wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, alisema magonjwa yanayowasumbua binadamu yapo ya aina mbili ambayo ni ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.
Dk Makalla alisema kundi la magonjwa ya kuambukiza ikiwemo malaria, tumbo na homa mengi yanatokana na kutozingatia usafi.
“Hakuna njia yoyote unaweza kukinga magonjwa yasiyo ya kuambukiza bila kuzingatia usafi binafsi, usafi wa mazingira, malazi na vyakula ni ngumu kutokomeza, ndiyo maana kadri kipato kinavyoongezeka na elimu kuwa juu yanapungua,”alisema.
Alisema athari ya ugonjwa wa malaria kwenye jamii kwa sasa sio kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, akisisitiza chanzo kikubwa cha magonjwa ya kuambukiza ni umasikini.
Analitaja kundi lingine la magonjwa ambayo ni yale yasiyoambukiza (magonjwa sugu) ambapo kadiri uchumi wa nchi unavyokuwa ndipo mfumo wa maisha ya binadamu hubadilika jambo linalochochea ongezeko la magonjwa hayo.
Anatolea mfano, “Miaka ya nyuma watu walikuwa wanachemsha viazi sasa wanakaanga na kila mtaa wanauza vyakula vya mafuta mengi, kwa hiyo kumekuwa na ulaji usio sahihi na jamii kutofanya mazoezi.
Ukiangalia magonjwa yanayoitia Serikali hasara ni yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la juu la damu na tatizo la moyo, sasa ni namna gani kukabiliana nayo ni kubadili mfumo wa maisha kwa kufanya mazoezi na kuangalia aina ya vyakula tunavyokula,”alisema.
Naye, Dk Ford Chissongela wa kliniki ya Hafford Health Care iliyopo Temeke, alisema uzingatiaji wa usafi katika chakula ni njia mojawapo ya kuepuka magonjwa hayo.
“Nashauri mtu akijisikia dalili za homa aende hospitali akapate tiba asisubiri aumwe zaidi, watu wengi wanaodharau kupata matibabu mapema wanarudi hospitali wakiwa wamezidiwa wanaishia kulazwa,” alisema.
Akizungumzia magonjwa ya njia ya hewa, Dk Ford alisema chanzo chake ni msongamano mkubwa wa watu, hivyo alishauri misongamano isiyo ya lazima iepukwe.
Alisema ni muhimu watoto wakaepushwa na misongamano isiyo ya lazima, kwa sababu kundi hilo lipo kwenye hatari zaidi ya kupata magonjwa ya mfumo wa hewa.
“Tuepuke kuishi kwenye nyumba ndogo watu wengi, tujitahidi kuishi kwenye nyumba zenye dirisha la kupitisha hewa ya kutosha,” alisema.
Kwa upande wake, Dk Zainabu Hussein wa Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa, alisema magonjwa ya presha na kisukari yanaongoza kwa sasa kutokana na wagonjwa kutozingatia dawa na mtindo sahihi wa maisha.
“Wagonjwa wa maradhi haya wanaacha kutumia dawa na wakifika hospitalini tayari wanakuwa na hali mbaya, hivyo lazima umpe kitanda ili umchunguze hali yake hadi akae sawa,” alisema.
Alisema licha ya malaria kuonyesha yamepungua katika takwimu, lakini mara nyingi mgonjwa akigundulika kuwa nao unakuwa mkali sana na analazimika kupewa kulazwa.
“Magonjwa ya tumbo yanalaza sana wanawake kwa sababu sasa hivi wengi wanapata maumivu makali chini ya tumbo na mtu kama huyu huwezi kumruhusu aondoke lazima umuangalie mwenendo wake,” aliongeza.
Katika hotuba ya bajeti ya wizara ya afya ilitaja kuwepo kwa ugonjwa wa mfumo wa mkojo (UTI) kuwa ni miongoni mwa magonjwa 10 yanayosumbua Watanzania.
“UTI zimegawanyika katika makundi mawili kuna acute (ambayo ukiitibu hairudii tena) na kuna chronic ambayo inahitaji sindano.
“Wengi wanaugua ‘acute’ ambayo haihitaji kulazwa lakini ukibainika una ‘chronic’ lazima upewe kitanda ili daktari achunguze mwenendo wa ufanyaji kazi wa dawa na sindano,” alisema Dk Zainabu.
Naye Dk Juma Fea wa Zahanati ya Mbagala Kizuiani anasema magonjwa yanatofautina kutokana na eneo husika.
“Katika mazingira ninayofanyia kazi mara nyingi wagonjwa wenye sifa za kulazwa na tunaowapokea ni wenye Malaria, presha, kisukari, nimonia kwa watoto na uvimbe hivyo tunawapa rufaa,”alisema.
Mfamasia Mkuu wa Serikali afafanua
Kwa upande wake, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi alisema magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza yote yanapewa kipaumbele katika utoaji matibabu.
“Magonjwa yaliyotajwa katika taarifa (malaria, matatizo ya uzazi, homa, tumbo na mapafu) pia ndio kipaumbele katika matibabu.
Hivyo muongozo wa matibabu unatambua magonjwa hayo na kuaininisha matibabu yake,” alisema.
Msasi alisema wingi wa utoaji dawa husika unategemea na uhitaji wake kwa muda husika kwenye jamii. “Pia dawa na bidhaa za afya zilizopewa kipaumbele kupima upatikanaji wake zinazingatia magonjwa hayo. Uhitaji wake na uwingi wake hutegemea matokeo,” alisema.
Mwananchi