MJUMBE wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Azavel Lwaitama, amedai wanachama 19 waliofukuzwa na chama hicho walimtesa Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, kufuatia uamuzi wao wa kuukubali ubunge viti maalum kinyume cha sheria. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Dk. Lwaitama ametoa madai hayo leo tarehe 10 Machi 2023, akihojiwa maswali ya dodoso na Wakili wa wabunge hao wa viti maalum, Ipilinga Panya, katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu, jijini Dar es Salaam, mbele ya Jaji Cyprian Mkeha.
Alitoa madai hayo baada ya video yenye hotuba ya Mbowe akimtaka kiongozi wa wabunge hao, Halima Mdee, kuomba radhi kwa hatua waliyofanya mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Chadema.
Kufuatia hotuba hiyo, Wakili Panya, alimhoji ni utaratibu wa kawaida wa Chadema kurekodi video katika mikutano yake wakati inaendelea.
Ambapo Dk. Lwaitama alijibu “sababu siku hizi watu wanarusha moja kwa moja mitandaoni kusikiliza hotuba, baadae sijui kama ilirekodiwa kwa ajili ya kuletwa mahakamani.”
“…inaeleza mateso aliyopata Mbowe kuomba warudi kwenye kundi na kuwaomba watubu kurudi kwenye kundi, turudi kwenye kazi,” amedai Dk. Lwaitama.
Alidai Mbowe alimuomba Mdee kuomba radhi kwa kuwa alikuwa na uwezo wa kuwashawishi wenzake waombe radhi.
Dk. Lwaitama amedai kuwa, Mbowe alikuwa anajaribu kuwashawishi waombe radhi ili asiwapoteze lakini ilishindikana.
Kikao hicho cha Baraza Kuu la Chadema, kilifanyika Mei 2022, ambapo kilitupilia mbali rufaa ya wabunge hao kupinga kuvuliwa uanachama.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa mahakamani halo mbele ya Jaji Mkeha, ambapo Dk. Lwaitama anaendelea kuulizwa maswali ya dodoso na Wakili Panya, kuhusu hati kiapo kinzani walichowasilisha mahakamani kujibu malalamiko ya kina Mdee.
Mdee na wenzake wamefungua kesi hiyo Na. 36/2022 mahakamani hapo, kupinga kufukuzwa Chadema bila kupewa nafasi ya kusikilizwa.
Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online.