Mama Aliwa na Mamba akiogelea Ziwa Victoria, Aacha Watoto Sita yatima





Buchosa. Editha Ndakadi (36) mama wa watoto sita Mkazi wa Kijiji cha Kanoni Kitongoji cha Bwego, Kata ya Maisome, Halmashauri ya Buchosa Wilaya Sengerema mkoani Mwanza amepoteza maisha Februari 9 mwaka huu kwa kushambuliwa na mamba na kuacha watoto sita wakati akioga Ziwa Victoria.

Mama huyo ni miongoni mwa watu saba waliopoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba kuanzia Januari Mosi mwaka huu 2023, huku sita wakiwa wakazi wa Kata ya Nyasasa Kisiwa cha Kome.

Hayo yamebainika kwenye kikao cha baraza la madiwani kikao cha robo ya pili ambapo Diwani wa Kata Nyakasasa, Deogratius Ivoy kuibua hoja ya vifo vya wananchi kupotezea maisha kwa kushambuliwa na mamba ambapo hoja hiyo imeungwa mkono na Diwani wa Kata ya Maisome, Damsoni Miyaga na kuthibitisha kutokea kwa tukio katika kata yake la mama aliyeshambauliwa na mamba wakati akioga Ziwa Victoria.

Baraza hilo la Madiwani la Halmashauri ya Buchosa limeiomba serikali kuruhusu watu wanaotumia mira za jadi kuvuna mamba hao kutokana na maofisa wanyapori wanapokuwa wakiwawinda mamba hawaonekani na kushindwa kufanikisha zoezi hilo.


Matukio ya mamba kuwashambulia wananchi kisha kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa kudumu imekuwa kama ajenda ya kudumu wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza hasa Halmashauri ya Buchosa anayozungukwa na maji kwa asilimia 80.

"Wananchi wetu wanapoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba tunaona serikali utusaidie katika jambo hili ili tuokoe nguvu kazi,” amesema Miyaga.

Kaimu mkurungenzi wa Halmashauri ya Buchosa Mwita Waryoba licha ya kusikitishwa na matukio hayo ameliambia baraza la madiwani kutoa vibali kwa wananchi ili kukabiliana na mamba hao, huku akiwaomba madiwani kutoa elimu juu ya Sumu ya Mamba pindi wanapokuwa wameuwawa isilete madhara kwa wananchi.


Mkuu wilaya ya Sengerema Senyi Ngaga amesema Serikali italifanyia kazi jambo hili na wananchi waweze kufanya shughuri zao bila woga.

Usuli

Matukio ya mamba kushambuliwa wananchi kisha kuuwauwa na wengine kupata ulemavu wa kudumu imekuwa kama ajenda ya kudumu kwenye vikao vya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Buchosa ambapo wameiomba serikali kuchukulia jambo hili kama dharula ili kuokoa maisha ya watu.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad