Mamia wamzika Neema, baba ahusisha kifo na kazi yake



Moshi. Baba mzazi wa Neema (Martha) Towo aliyekufa kwa madai ya kuchomwa moto wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani, Ndeonasia Towo amehusisha kifo cha mwanaye huyo na masuala ya kazi.

Pia, Towo amedai kuwa katika eneo la tukio alikochomwa mwanaye, kulikuwa na vichupa vya dawa vinavyodhaniwa kuwa na sumu.

Towo aliyasema hayo jana alipozungumza na Mwananchi baada ya mazishi ya mwanaye huyo nyumbani kwao katika kijiji cha Mrimbo Uuwo, Mwika wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Neema anadaiwa kutekwa na kuuawa kwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana Machi 3 mwaka huu, ambapo Towo alieleza juzi kuwa siku ya tukio mwanaye alikuwa kanisani kwenye ibada ya jioni ambapo alipigiwa simu na watu asiowajua akiwa ndani ya kanisa, alitoka nje kusikiliza baada ya hapo hakuonekana tena.


Akizungumza jana katika mazishi hayo, Towo alihusisha mauaji ya mwanaye na masuala ya kazi.

“Personally (binafsi) ni suala la kikazi na Neema hakuwa na maadui wowote, Neema nimekaa naye na amenitembeza sehemu mbalimbali, hana maadui,” alisema.

Alisema bado uchunguzi unaendelea na kwamba suala la kuuchunguza mwili ni suala la kitaalam.


“Postmortem (uchunguzi wa mwili wa marehemu), ni jambo la kitaalamu sana ambapo majibu yake yanatolewa na mamlaka husika,” alisema.

Aliendelea: “Baada ya mgonjwa kuletwa Hospitali ya Tumbi na Polisi jamii na raia wema, askari waliondoka na wale ndugu waliomleta, wakaenda kwenye eneo la tukio.

“Kuna baadhi ya vielelezo walivyopata ambavyo ni pamoja na vichupa vya dawa, kwa hiyo kuna uwezekano, moto peke yake usingeweza kumwathiri hivyo.

Vichupa hivyo vilikuwa vimevunjwa, kukiwa na chupa ya mafuta ya taa na chupa ya petrol, kwa hiyo pamoja na moto, kuna dawa zitakuwa zimemwongozea.


Hata hivyo, alisema dawa hizo hazikuletwa hospitali.

“Rai yangu kwa Serikali, ni kuweka vipindi maalum, kwa sababu kila kunapokucha kuna tukio la kiharamia, ni kweli tumeshindwa kuingia kwenye ngazi ya familia na kutoa funzo kama hilo.

“Kwa mfano, mtoto wangu huyu ameokolewa na Polisi Jamii, kwa hiyo tuweke kama ilivyo balozi, polisi wawepo kila kona ndio kitu pekee kitakachotusaidia,” alisema.

Hata hivyo, akizungumza juzi na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo alisema chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika na bado wanaendelea na uchunguzi.


Alisema baada ya Neema kukutwa akiungua moto alipelekwa hospitali ya Tumbi na wasamaria wema.

‘‘Mgonjwa alihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uangalizi zaidi wa kimatibabu, lakini alifariki Alhamisi Machi 9,” alisema.

Jana alipotafutwa kwa simu, Kamanda Lutumo hakupokea licha ya simu yake kuita kwa muda mrefu.

Vilio vyatawala

Katika msiba huo, vilio na simanzi vilitawala katika mazishi ya binti huyo aliyewahi kufanya kazi benki ya BOA.

Msiba huo uliosafirishwa kutoka Kibaha Pwani kuelekea mkoani Kilimanjaro, ulihudhuriwa na mamia ya waombolezaji waliotokea ndani na nje ya mkoa huo.


Awali akizungumza katika ibada ya mazishi, Towo aliliomba kanisa limwombee kwa kuwa familia yake imepitia katika wakati mgumu wa kuondokewa na mtoto wao aliyeuawa kikatili.

“Mniombee kwa sababu nitalazimika kwenda kufuatilia haki za mwanangu pamoja na mambo mengine.Mniombee maana pia napitia katika changamoto kubwa ya kuondokewa na mtoto wetu mpendwa aliyekuwa jasiri na aliyejituma,” alisema.

Akitoa mahubiri wakati wa ibada ya mazishi katika kanisa la KKKT, Usharika Uuwo, Mwika wilaya ya Moshi, Mwinjilisti John Ngowi alisema mauaji hayo hayapaswi kuvumilika na kwamba hakuna mwenye haki ya kuondoa uhai wa mwenzake.

Alisema maisha ya Neema yamehitimishwa kikatili na kwamba ni jambo ambalo halikubaliki katika jamii yoyote ile kwani Mungu ndiye anayejua mwisho wa maisha ya mtu pekee.

“Maisha ya Neema yamehit kikatili, hili halikubalika katika jamii yoyote ile kwani Mungu anataka watu wote waishi mpaka hapo Mungu alipoweka kikomo cha mtu kuishi hapa duniani,”

Alisema kitendo hicho ni chukizo mbele ya Mungu na kwamba yupo Mungu mtetezi asimamaye akiwatetea wale waliodhulumiwa uhai wao.

Akisoma historia ya Marehemu, kaka wa Neema, Nelson Towo alisema dada yake huyo wakati wa uhai wake, alifanya kazi katika sehemu mbalimbali na kwamba alikuwa ni mtu shupavu na aliyejituma katika kazi.

“Mwaka 2015 hadi 2016 alifanya kazi katika kampuni ya M-pawa ambapo 2016 hadi 2017 alijiunga na NMB akihudumu nafasi ya Ofisa Mauzo NMB chapuchapu mkoani Manyara,

“2017 mwishoni hadi 2023 aliajiriwa na Benki ya BOA Babati, Manyara kwa nafasi ya Ofisa Ushirikiano na alifanya kazi vizuri na baadaye alihamishwa kituo cha kazi kutoka Babati kwenda Kahama ambapo alipandishwa cheo na kuwa, Meneja Uhusiano,”

Naye Diwani wa Kata ya Mwika Kaskazini, Samuel Shao ambaye pia ni ndugu wa marehemu Neema, akiwa kanisani hapo, aliviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuharakisha uchunguzi wa mauaji ya ndugu yao.

Alisema hayo ni kulingana na maagizo ya Rais ya kuvitaka vyombo hivyo kutochelewesha majibu ya kile wanachokichunguza ili kuondoa wasiwasi.

‘‘Tunaomba haki za huyu binti yetu iweze kupatikana na kama Kuna kitu ambacho kimefanyika kijulikane,” alisema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad