Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imefanya utabiri wa hali ya hewa wa siku tano huku ikitoa angalizo kwa siku mbili za Machi 14 na 15, 2023 ambazo zinatarajiwa kuwa na mvua kubwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 13, 2023, angalizo la mvua kubwa limetolewa katika maeneo machache ya mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe, Rukwa, Katavi, Tabora, Kigoma, Singida, Dodoma na Ruvuma kwa Machi 14, 2023.
Machi 15, 2023, TMA imetoa angalizo la mvua kubwa katika maeneo machache ya mikoa ya Mara, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe, Rukwa, Katavi, Tabora, Kigoma, Singida, Dodoma na Ruvuma.
“Athari zinazoweza kujitokeza ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji pamoja na ucheleweshwaji wa baadhi ya shughuli za uchumi na usafirishaji,” inaeleza taarifa hiyo ya TMA.
Hata hivyo, hakuna tahadhari yoyote iliyotolewa kwa Machi 16 na 17, 2023 kwa kuwa hali itakuwa shwari katika mikoa yote ya Tanzania.
Wakati TMA ikifanya utabiri huo, baadhi ya maeneo ya Tanzania yanakabiliwa na uhaba wa mvua, jambo ambalo linahatarisha uzalishaji wa chakula kwenye maeneo hayo sambamba na malisho ya mifugo.