Msemaji wa Ikulu ya Marekani Karine Jean-Pierre ameonya Wabunge wa Bunge la Uganda kwamba vikwazo vitakavyowazuia kufanya biashara na Marekani vinaweza kuwekwa kwa wale wanaohusika na kupitishwa kwa sheria ya kuwafunga wanaofanya mapenzi ya jinsia ya moja na uhalifu wa kundi la LGBTQ+.
Jean-Pierre ametoa maoni hayo mapema wiki hii katika Mkutano na Waandishi wa Habari ambapo amesema Ikulu ya Marekani ilikuwa ikiangalia kinachoendelea nchini Uganda kwa umakini na kuangalia maamuzi ya hatua ambazo Marekani zitachukua iwapo sheria hiyo itatiwa saini na kuanza kutumika.
Muswada huo uliopitishwa na Bunge la Uganda utatekeleza hukumu za kifungo cha hadi miaka 10 jela kwa yeyote atakayepatikana na hatia ya aina mbalimbali za vitendo vya ushoga nje ya kanuni za Watu wa jinsia tofauti.
Baadhi ya vitendo vinavyochukuliwa kuwa ushoga uliokithiri vitastahiki hukumu ya kifo, iwapo utatiwa saini na Rais wa Uganda ambaye ana historia ya kukashifu jumuiya ya LGBTQ+ itaifanya Nchi hiyo kuwa moja ya Nchi zenye sheria kali zaidi duniani kwa Watu wa kikundi cha LGBT+, kikiwa ni kikundi ambacho kinaungwa mkono na serikali ya Marekani.
Watetezi wa haki za kibinadamu nchini Uganda wanasema sheria hiyo ni tishio la kuharibu uhusiano wa kiuchumi na Marekani pamoja na kukiuka haki za Binadamu na hili linaweza kutosha kumshinikiza Rais wa Nchi hiyo Yoweri Museveni kutokutia saini sheria hiyo.