Mshambulizi wembe Lionel Messi amekashifiwa vikali kufuatia Paris Saint-Germain kuondolewa kwenye mtanange wa Ligi ya Mabingwa.
Parisians walipata kichapo mfululizo katika hatua ya 16 Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya wakipigwa 3-0 na Bayern Munich.
Akipata umaarufu wake katika Kombe la Dunia, mshindi huyo mara saba wa tuzo ya Ballon d'Or alitarajiwa kubeba PSG kushinda UEFA sawia na alivyoongoza timu yake ya nyumbani Argentina kwa ushindi.
Lakini katika kipindi cha msimu wa pili mfululizo, Messi na wachezaji wenzake wa PSG hawatatinga tena UEFA, kulingana na ESPNFC.
Kichapo cha Jumatano, Machi 8, usiku mikononi mwa Bayern, kinaongeza masaibu ya wenyeji hao wa Paris katika shindano kuu la bara Uropa, GOAL inaripoti.
Mashabiki walivyomchamba Messi
@vibin_rajan aliandika: "PSG ilimsaini GOAT mbaya. Wangekuwa wameshinda UCL na GOAT sahihi kufikia sasa."
@Mohamed50695175 aliongeza: "Messi ameharibu PSG yangu ninayoipenda. Ni lazima aondoke, au tutamzomea tena."
@gyaigyimii aliandika: "Messi na Ronaldo watatazama fainali ya ligi ya mabingwa wakiwa nyumbani."
@UTDTrey aliuliza: "Swali tu, Messi alijitokeza lini mara ya mwisho katika mchezo mkubwa wa ligi ya mabingwa?"
Kocha wa PSG achemka
Kocha wa Paris Saint-Germain Christophe Galtier alikiri kuwa mabingwa hao wa Ufaransa hawana budi ila kukubali kuondolewa kwao mapema katika UEFA.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba matokeo hayo ya mechi ya marudiano ya hatua ya 16-bora dhidi ya Bayern Munich yangekuwa tofauti iwapo wageni wangefunga bao la kwanza katika mchezo huo.
"Ni jambo la kukatisha tamaa sana. Kwa bahati mbaya inabidi tuichague na kuikubali. Lazima tuendelee kwenye ligi. Kila mtu amekata tamaa, hata mimi. Hata kama tulikuwa na matatizo mengi katika mechi ya kwanza tuliweka matumaini makubwa katika mkondo wa pili," alilalamika kocha huyo.