Mchakato wa Katiba mpya waiva





MCHAKATO wa Katiba mpya pamoja na marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa na Uchaguzi unatarajiwa kuanza kufanyiwa kazi baada ya kupitishwa kwa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2023/24.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro aliyasema hayo jana alipokuwa akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi la wizara hiyo kilichofanyika jijini hapa.

Dk. Ndumbaro alisema marekebisho ya katiba yataanza kufanyika baada michakato ya kupitishwa kwa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kupitia baraza la wafanyakazi na mwisho kuidhinishwa na Bunge.

“Mchakato wa Katiba mpya ni agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo ili kufanikiwa unahitaji rasilimali fedha nyingi na wajumbe wa kikao cha baraza la wafanyakazi mtambue mna jukumu hilo la kupitia mapendekezo ya bajeti ya mwaka huu 2023/24 ili kufanikisha mambo hayo makubwa ya kitaifa,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Ndumbaro, hitaji la Katiba mpya ni la Watanzania, hivyo  wizara yake inatakiwa kujipanga ili kuhakikisha inakamilisha mchakato huo kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwakani na uchaguzi mkuu mwaka 2025.


“Marekebisho ya sheria za uchaguzi hizo yanahitajika pamoja na Sheria ya Tume ya Uchaguzi, hivyo wizara yetu inahitaji rasilimali fedha kupitishwa ili kukamilisha michakato hiyo haraka,” alisema.

Alibanisha kuwa mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni Sh. bilioni 36 sawa na ongezeko la Sh. bilioni tisa ya fedha zilizoidhinishwa na bunge kwa mwaka wa fedha unaomalizika.

Pia alisema wajumbe hao wanahaki ya kuongeza au kupunguza mapendekezo hayo ili kukamilisha jukumu walilopewa na Rais kuhusu marekebisho hayo.

Aliyataja majukumu mengine waliyokabidhiwa kuwa ni kutumia majukwaa ya kimataifa kuhusu kuondoa dhana kuwa nchi haiheshimu haki hizo pamoja na kutoa elimu ya sheria kwa wananchi.

Waziri Dk. Ndumbaro alisema kuna mambo mengi yanayoihusu wizara hiyo ambayo yanahitaji fedha ili kukamilisha kwa wakati majukumu hayo makubwa ya kitaifa na kimataifa.

Aidha, aliwataka watumishi kujenga tabia ya kujiwekea akiba kabla ya kustaafu ili kuondoa malalamiko kwa wastaafu.

Dk. Ndumbaro alisema kuna baadhi ya watumishi wamekuwa na tabia ya kuishi maisha ya anasa wakiwa kazini lakini wakistaafu wanakosa akiba ya kuendesha maisha.


Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo na Katibu Mkuu wa Wizara, Mary Makondo, aliyataja malengo ya baraza hilo kuwa ni kupokea mapitio ya bajeti ya mwaka 2022/23 na mapendekezo ya bajeti ya fedha ya mwaka 2023/24.

Makondo alisema katika kikao hicho pia watajadiliana kwa pamoja masuala ya mafanikio na matatizo katika sehemu ya kazi ili kuondoa malalamiko.




Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad