Mchungaji afunga kanisa kisa Sh100 milioni za kamari



Dodoma. Sakata la mchungaji mmoja nchini Uganda (jina limehifadhiwa) aliyefunga kanisa baada ya kushinda Sh100 milioni kwenye mchezo wa bahati nasibu, limewaibua viongozi wa kiroho huku kila mmoja akija na mtazamo wa tofauti.

Machi 16, mwaka huu mtandao mmoja Uganda ulichapisha taarifa za mchungaji huyo akieleza kuwa ameamua kufunga kanisa lake ili afanye shughuli nyingine kwa kuwa amepata fedha nyingi.

Mtandao huo ulimnukuu mchungaji akieleza namna alivyocheza bahati nasibu ya Sh1 milioni lakini akashinda Sh100 milioni ambazo hakutarajia kama angepata.

“I must admit that I opened this church due to greed but not anointing (lazima nikiri nilifungua kanisa hili kwa sababu ya ‘uchoyo’ lakini sio upako) inasema sehemu ya habari hiyo ikimnukuu mchungaji huyo.


Mchungaji huyo alisema ilimlazimu kuacha kanisa kwa sababu alikuwa na njia zake za kupata pesa na hadi sasa ameshafanya mambo mengi ambayo hakuwahi kufikiria kama angeweza kuyafanya maishani mwake.

Maoni ya wachungaji

Wakizungumzia kisa hicho pamoja na tabia ya baadhi ya viongozi wa dini kufungua makanisa kwa lengo la kujichumia utajiri, baadhi ya viongozi wa dini wamesema matukio hayo yapo.

Mwenyekiti wa Umoja wa Madhehebu mkoani Dodoma, Askofu Anthony Mlyashimba alisema tukio hilo ni la ajabu lakini haliwezi kuwa la kwanza, kwa kuwa wako wachungaji wengi wanaofanya mambo kama hayo.

Askofu Mlyashimba ambaye anahudumu katika Kanisa la Baptist alisema kitendo kilichofanywa na kiongozi huyo hakithibitishi utume kwake kwamba alikuwa amechaguliwa kwa ajili ya kuwatumikia waumini, bali alitaka kujitafutia fedha.

Kiongozi huyo alisema kuibuka kwa watu wanaojiita watumishi wa Mungu hivi karibuni, ni lazima waumini wachague kwa kuwapima, vinginevyo yatakuja kutokea majanga.

“Kwanza mtu wa Mungu kucheza kamari sio kitendo chema, lakini Biblia inasema tutawatambua kwa matendo yao sio maneno na huyo alishakuwa mtu wa namna hiyo,” alisema Askofu Mlyashimba.

Mchungaji Ezer Laitoti wa Kanisa la EAGT Kiteto, alisema kitendo cha mtu kucheza kamari, ni wazi alikuwa ameacha muda wa kusoma na kutafakari neno lakini anawaza habari za lini atashinda fedha.


“Huyu angeweza hata kuiba ilimradi tu apate fedha, hii sio sawa kwangu mimi hata kidogo, lazima tuwatambue watu wa namna hii na waumini wetu wawe makini sana,” alisema Laitoti.

Mwinjilisti Naomi Hosea wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mpwapwa, alisema alichofanya mchungaji wa Uganda hata Tanzania kipo, isipokuwa watu hawajaripoti.

Naomi alisema, “hii ni sawa na dereva wa gari, ukiwa msafiri huwezi kumuuliza leseni yake akiwa barabarani, unajua ni mtu sahihi, kumbe kikosi cha usalama ndiyo wanatakiwa kutambua hilo na kuwazuia wasiofaa, na hili Serikali iwe macho nacho ili watusaidie.”

Polisi

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Miseme alisema matukio kama hayo hawajawahi kukutana nayo ingawa yanaweza kuwepo kwa uchache sana.

Misime alisema ni uhuru wa mtu kuabudu na ndiyo maana polisi haiwezi kuingilia kwa ajili ya kuwabaini wanaokwenda kinyume isipokuwa wakisikia wanakwenda kuhoji.

“Hapa kwetu labda kama uvunjifu wa haki za watoto kwa baadhi ya watu wanaohubiri, hayo kwa uchache tumeyapokea, lakini kinyume na hapo ni imani za watu wenyewe sisi hatuingilii,” alisema Misime.

Hata hivyo, alisema hakuna sheria kamili kama alivyowahi kusema aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene kwamba kunapaswa kutungwa sheria ya kudhibiti usajili wa makanisa.

Kwenye hoja hiyo, Simbachawene alikuwa akizungumzia waumini 20 waliopoteza maisha mkoani Kilimanjaro walipokuwa wanagombania kukanyaga mafuta ya upako, ndipo akasema ni muhimu kuangalia usajili wa makanisa na kiwango cha waongozaji katika elimu.

Polisi mstaafu, Joshua Halanja alisema kwa sasa kinachopaswa kudhibitiwa ni wahubiri wanaotembea na vipaza sauti na kuhubiri neno la Mungu kwenye masoko na mikusanyiko kisha wanaomba sadaka.


Joshua alisema ni ngumu kuwadhibiti watu wa namna hiyo, lakini Serikali ikiwawekea sheria mara moja wataacha.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad