Dar es Salaam. Shangwe na nderemo vimetawala katika Kanisa la KKKT Usharika wa Kijitonyama wakati wa ibada ya asubuhi (morning Glory) baada ya mchungaji Dk Eliona Kimaro kuwasalimia waumini na kuwashukuru.
Usiku wa Januari 16, 2023 ilisambaa video ikimuonyesha mchungaji Kimaro akiwaeleza waumini wake kuwa amepewa likizo ya siku 60 baada ya kuitwa katika ofisi ya msaidizi wa askofu na kufanya kikao na mkuu wa jimbo.
Dk Kimaro ambaye ni mchungaji kiongozi waa Usharika huo ameripoti usharikani hapo leo Ijumaa Machi 17, 2023 baada ya kumalizika kwa likizo ya siku 60.
Hata hivyo Februari 19 Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa alitangaza kumsamehe mchungaji Kimaro.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa ibada hiyo Dk Kimaro amewashukuru waumini wa usharika huo kwa uvumilivu kwa kipindi chote alichokuwa kwenye nyumba ya malezi huku akitangaza ratiba za ibada ya Kwaresma kwa siku zilizobaki.
Waumini walioshiriki ibada hiyo wameshindwa kujizuia kwa furaha walizokuwa nazo kila alipokuwa akizungumza walinyanyuka na kushangilia na wengine kurusha maua.