Msafara wa ACT -Wazalendo wapokewa na ndoo tupu za maji



MSAFARA wa Chama cha ACT - Wazalendo ukiwa katika Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, umepokewa na wananchi waliokuwa na ndoo tupu za maji, wakiashiria kuomba kusaidiwa kutatua kero hiyo.

Zitto Kabwe.
Wananchi hao waliokusanyika katika viwanja vya Wananchi Square mjini hapo,  walimweleza kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, kwamba awasaidie kuwatua ndoo kichwani kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta maji.

Kwa mujibu wa Zitto, awali ilielezwa kwamba yatatolewa maji katika Mto Malagarasi Kigoma kwa ajili ya Urambo na Kaliua na pia ilitolewa kauli nyingine kuwa mradi wa maji Ziwa Victoria unaopeleka maji Tabora utafikisha pia Urambo.

"Kwa hiyo nimeshtuka nafika hapa napokewa na ndoo kwamba mradi haujafika Urambo na bado wananchi wana kero ya maji ya miaka yote," alisema Zitto.

Alisema tatizo la maji katika mji wa Urambo ni la muda mrefu na jambo la kushangaza ni kwamba serikali haijalipa uzito kwa kuleta ufumbuzi na wananchi hao kupata maji kupitia miradi inayotekelezwa.


Kutokana na hali hiyo, Zitto alitoa wito kwa Waziri wa Maji, Juma Aweso kushughulikia suala la maji katika mji wa Urambo kwa haraka iwezekanavyo kwa kueleza mradi utakaowanufaisha wananchi hao.

"Namtaka Waziri Aweso aje Urambo aeleze ni mradi gani utatatua tatizo hili la muda mrefu. Atoe taarifa tujue Urambo itafaidika na mradi wa maji wa Ziwa Victoria wa Tabora au mradi wa Malagarasi tufahamu ni mradi upi ambao Urambo utafaidika nao kwenye miradi ya maji.

"Kila wakati tunahamishwa tu sasa Waziri wa Maji awaeleze wananchi ni mradi upi utamaliza tatizo la maji ni aibu sana mji kama huu, wilaya ya zamani hadi sasa haina maji ni jambo ambalo halikubaliki," alisema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad