Msuva, Samatta juu kwa juu Misri



NYOTA wa kimataifa wa Simon Msuva anayekipiga Al-Qadsiah FC ya Saudi Arabia pamoja na nyota wengine wanaocheza nje ya nchi walioitwa Taifa Stars wanatarajiwa kukutana juu kwa juu nchini Misri wakati timu hiyo itakapojiandaa kukabiliana na Uganda nchini humo.

Stars inatarajiwa kuvaana na Uganda kwenye mechi ya Kundi F itakayopigwa Misri Machi 24 kuwania fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zitakazofanyika mwakani nchini Ivory Coast na wachezaji hao walio nje wamepangiwa kuungana na timu huko huko badala ya kuja hapa nchini.

Mbali na Msuva wengine ambao wataunga na Stars ikiwa Misri ni Himid Mao 'Ninja' anayecheza soka la kulipwa nchini humo, Mbwana Samatta, Kelvin John na Novatus Dismas (Ubelgiji), Haji Mnoga na Ben Starkie (England) na Ramadhan Makame ambaye anatokea Uturuki.

Akizungumza na Mwanaspoti, Msuva alisema wameipania mechi hiyo  itakayochezwa Ijumaa ya Machi 24 kwenye Uwanja wa Suez Canal, Misri kwa kutambua ndiye itakayotoa dira kwa timu hiyo kwenda Ivory Coast kabla hata hawajarudiana Machi 28 jijini Dar es Salaam.

"Kama mshambuliaji ni jukumu langu kufunga hivyo huwa natamani kwenye kila mchezo kuwa sehemu ya matokeo ambayo timu yangu imepata, tunamchezo mkubwa na mgumu mbele yetu lakini kwa bahati nzuri tutacheza na timu ambayo tunaifahamu vizuri,

"Uganda ni majirani zetu mbali na sisi kuwafahamu nao wanatufahamu vizuri, tunatakiwa kuwa macho na makini kwenye mchezo huo ili tupate pointi ambazo zitatuweka sehemu nzuri, inawezekana kufanya vizuri kwenye mchezo huo kwa sababu wote tutacheza ugenini japo kiratiba Uganda inaonekana kuwa mwenyeji wa mchezo," alisema Msuva.

Msuva ambaye anatarajiwa kuungana na kikosi cha Adel Amrouche nchini Misri mara baada ya kulichezea chama lake wikiendi hii, aliongeza kwa kusema,"Kuendelea kukua kwa ligi yetu ya nyumbani na uzoefu wa wachezaji ambao wamekuwa wakicheza nje ya nchi, vinaweza kuongeza kitu kwenye timu yetu ya taifa."  


Stars kwa sasa inashika nafasi ya tatu kundini nyuma ya vinara Niger yenye pointi mbili na Algeria inayoongoza kundi na pointi sita kila timu ikiwa imecheza mechi mbili, ikusanya pointi moja sawa na Uganda inayoburuza mkia.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad