Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 60 anayefahamika kwa jina la Venantie Uwambaza, ameibua gumzo baada ya kusimulia stori yake ya mapenzi yenye kusisimua na kuhuzunisha, akidai kuwa hakuna mwanamume aliyewahi kumpenda kikweli kutoka ndani ya moyo wake.
Mama huyo ambaye yuko singo amebainisha kuwa amekuwa na uhusiano kadhaa na wanaume tofauti, lakini hakuna hata mmoja aliyewahi kumfikisha kwenye kilele cha harusi.
Alifichua kwamba mahusinao yote yaliishia katika machozi kwani wengi walisema hawakuwa kwenye mahusiano naye rasmi bali walikuwa wakipoteza muda na kumtumia kujiburudisha.
"Endapo katika miaka hiyo yote ningepata mtu anayenipenda tungekuwa tumeoana. Nilihitaji mtu wa kusema ananipenda. Na wale ambao nilidhani wananipenda hawakunipenda. Wengi walikiri kuwa wanapitisha muda," Venantie Uwambaza amesema.
Alikumbuka mpenzi wake wa kwanza alipokutana na mwanaume na kumpa ujauzito katika uhusiano wao akiwa mdogo. Siku moja, baada ya kutoka nje kwa muda, alirudi nyumbani na kukuta mlango umefungwa na jamaa huyo. Mpenzi huyo alikana ujauzito huo, na kumlazimu Uwambaza kurudi nyumbani kwa baba yake, ambako alipokelewa kwa furaha.
Alifichua tangu wakati huo, maisha yake ya uhusiano yalizidi kuzorota kwani kila mwanaume aliyekutana naye alisema walikuwa wakipitisha muda tu.
"Wengine walikuwa wakinilisha, walinilipa kodi, walininunulia nguo, wakinitunzia mtoto wangu na nilifikiri tunapendana. Wengine tulizaa nao watoto lakini walikiri kuwa hawakunipenda kwa dhati," alifichua.
Ilifika wakati akapata bahati ya kwenda nchini Marekani, ambapo alianza upya maisha yake, yalibadilika alipata pesa, gari nzuri na maisha mazuri. Licha ya kila kitu maishani, alikosa upendo wa dhati ambao moyo wake ulitamani.
Alikua mlevi kwa sababu ya mfadhaiko, kukatishwa tamaa na hata kuambukizwa ugonjwa wa Ukimwi ambao uliwaweka mbali watu wengi. Uwambaza hakuwa na uhakika kama atapata upendo tena, lakini aliwahimiza wanawake wengine wasikate tamaa.