Nape afunguka kilichogharimu uwaziri wake




Morogoro. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amevunja ukimya wa muda mrefu tangu alipozuiwa wakati anakwenda kuwaaga wanahabari baada ya kutenguliwa kufuatia sakata la kuvamiwa Kituo cha Clouds Media Group mwaka 2017.

Machi 2017, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alidaiwa kuvamia kituo hicho usiku akiwa na askari waliokuwa na silaha wakati kipindi cha ‘Shilawadu’ kikiendelea.

Jana, akifungua mkutano wa 12 wa kitaaluma wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) mkoani Morogoro, Nape alisema: “Sijawahi kusema, niliambiwa nikienda (kuchunguza uvamizi wa Kituo cha Clouds Media Group) utakuwa huna kazi, lakini nilisema bora nisiwe na kazi lakini nilinde heshima yangu.”

Tukio la uvamizi huo lilipingwa na kulaaniwa na wadau mbalimbali, huku Nape, aliyekuwa Waziri wa Habari wakati huo, akiunda kamati ya kuchunguza suala hilo aliloishia kupokea ripoti yake na kabla ya kuiwasilisha kwa mamlaka husika ya uteuzi, alitenguliwa uwaziri.


Machi 23, 2017, ikiwa ni saa chache kupita tangu aliyekuwa Rais wa wakati huo, John Magufuli kumwondoa katika baraza lake la mawaziri, Nape alipanga kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, alikutana na zuio la vyombo vya dola na alipolazimisha alijikuta akitolewa bastola mbele ya waandishi huku akitakiwa kurudi ndani ya gari lake na asifanye mkutano huo na wanahabari.

Septemba 10, 2019, Nape alisema alikwenda Ikulu, Dar es Salaam kuomba radhi kwa Rais John Magufuli, ambapo haikuwa rahisi kukutana naye.


Hata hivyo, alifanikiwa kukutana na kiongozi huyo na kutangaza kwamba, amemsamehe Nape ikiwa ni muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo yao.

Jana, Waziri Nape alisema: “Niliamua kuchagua heshima kwa kuwa utaenda nayo, lakini kazi ipo siku itaondoka, kwa hiyo nikachagua heshima ambayo nadhani ndio naendelea kuwa nayo na hii ndio sababu ya hata leo mmeamua kunipa tuzo hii.

“Baada ya pale tukaunda timu ya uchunguzi ambayo (Deodatus) Balile (Mwenyekiti wa TEF) alikuwa mjumbe, baadaye wakati tukikutana pale Habari Maelezo tukitaka kusoma taarifa ya ripoti tulishauriana na timu ikiongozwa na (Hassan) Abbas na Jesse (Kwayu) tukawa tunaambiana tusome au tusisome.”

Alisema kabla ya kwenda kukutana na timu hiyo alipitia mahali na kuwaeleza kuwa taarifa ipo tayari na alikuwa akisubiriwa na wale watu walimtaka aamue kuisoma, kuondoka au kuinyamazia ili aendelee na kazi na kutafakari kuchagua kuendelea na heshima.


“Leo nimesema niseme, ndio maana hata lilipotokea haikuwa shida kwangu kwa sababu nilijua na wakati napokea taarifa niliwaambia hawa kuwa, kuna gharama ya kulipa kwa hiki nilichofanya. Kwa hiyo wakati mwingine sio rahisi sana lakini nafurahi leo tasnia ya habari inaendelea kuwa bora na ninasikia fahari kujenga heshima,” alisema Nape, ambaye Rais Samia Suluhu Hassan alimteua kushika wadhifa huo.

Akizungumzia masuala ya sheria, alisema anatarajia kuona wanatunga sheria itakayodumu kwa miaka 50 hadi 100 na kuwataka waendelee na mjadala kwa kuwa Serikali ipo tayari kuwasikiliza muda.

Awali, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alisema idadi ya kesi zinazopelekwa mahakamani dhidi ya vyombo vya habari imepungua kwa kiasi kikubwa, kwa sasa imefikia mwaka mzima bila chombo cha habari chochote nchini kufunguliwa kesi na mtu binafsi au Serikali.

Alimshukuru Rais Samia kubadili upepo na mwelekeo wa utendaji wa vyombo vya habari nchini.


Balile alisema tangu Rais Samia aingie madarakani, kumekuwapo ushirikiano mkubwa kati ya vyombo vya habari na Serikali.

Hata hivyo, alisema kumekuwa na mchakato wa muda mrefu juu ya marekebisho ya sheria za habari kuwa na viwango vya kimataifa.

Alisema wanaishukuru na kutambua marekebisho yaliyopendekezwa na Serikali, ikiwamo kufuta kashfa kugeuzwa jinai na marekebisho hayo yataifanya Tanzania kurejesha heshima yake.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad