Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema aliamua kuchagua heshima badala ya cheo chake wakati wa uchunguzi wa sakata la uvamizi wa kituo cha habari cha Clouds Media Group uliodaiwa kufanywa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda mwaka 2017.
Akisimulia kisa hicho, Nape ambaye wakati huo alikuwa akihudumu kama Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema wakati alipounda tume ya uchunguzi ndani ya saa 24 kuchunguza tukio hilo, alizuiwa kufanya uchunguzi huo na kuambiwa kuchagua kati ya kuachana na uchunguzi au kufukuzwa kazi.
“Asubuhi yake nilizuiwa kwenda kuchunguza nikaambiwa ukienda utakuwa hauna kazi, nikasema ni bora nisiwe na kazi lakini nilinde heshima yangu,” amesema.
Hata hivyo, baada ya uamuzi wake wa kuchagua kuendelea na mkakati huo alitenguliwa katika nafasi yake siku moja baada ya kupokea ripoti ya kamati ya uchunguzi na aliyekuwa Rais wa awamu ya Sita, Hayati Dkt. John Magufuli.