Msanii wa muziki wa hip hop Hubert Nakitare, almaarufu Nonini ameshinda kesi ya kisheria dhidi ya kampuni ya Kijapani ya Syinix electronics na mshawishi Brian Mutinda kwa kutumia wimbo wake bila kibali, na kuweka historia kubwa katika uchumi wa ushawishi nchini Kenya.
Washtakiwa hao waliamriwa na Mahakama ya Milimani mnamo Alhamisi kumlipa Nonini KES milioni 1 fidia ya jumla kwa kukiuka hakimiliki yake.
Kesi hiyo ilitokana na video ambayo Mutinda alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram mnamo Aprili 2022, akitangaza TV mpya ya skrini bapa kutoka Syinix.
Video hiyo iliangazia wimbo maarufu wa Nonini "We Kamu", ambao ulisawazishwa na taswira bila leseni kutoka kwa msanii huyo. Video hiyo hiyo pia iliwekwa kwenye ukurasa wa Facebook uliothibitishwa wa Syinix.
Mnamo Julai 2022, Nonini alikuwa amewaandikia Mutinda na Syinix akidai kulipwa fidia na kuomba msamaha. Pia alipost nyaraka za mahakama kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, akiwatahadharisha mashabiki wake kuhusu hatua hiyo ya kisheria.
Hata hivyo, washtakiwa hawakutekeleza ombi lake, hali iliyomfanya Nonini kuwasilisha kesi mahakamani kupitia mawakili wake Agosti 2022.
Syinix, kwa upande mwingine, alikanusha kutengeneza video yoyote iliyokiuka hakimiliki ya Nonini na kudai kuwa haifahamu haki zozote zinazohusiana na wimbo huo.
Hata hivyo, kampuni ilionyesha nia ya kujadili uwezekano wa kutoa leseni ya upatanishi ya "We Kamu" kwa Nonini.
Nonini anachukuliwa kuwa mmoja wa waanzilishi wa muziki wa mijini wa Kenya na godfather wa genge. Ametoa albamu kadhaa na kushirikiana na wasanii wa ndani na wa nje. Yeye pia ndiye mwanzilishi wa P-Unit (Pro-Habo Unit), kikundi cha rap ambacho kimeshinda tuzo kadhaa.