Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amelaani uvamizi wa mali ya aliyekuwa rais wa taifa hilo Uhuru Kenyatta.
Katika mahojiano na BBC kiongozi huyo wa upinzani alisema anaamini shambulio hilo lilitekelezwa na ‘majangili’ waliokodishwa na serikali.
Bw Kenyatta ni mshirika wa Odinga. Jumatatu ilikuwa siku ya pili ya maandamano dhidi ya serikali yaliyoitishwa na Bw Odinga kwa madai kwamba kulikuwa na udanganyifu katika uchaguzi uliopita pamoja na kupanda kwa gharama ya maisha nchini.
Kuporwa kwa shamba kubwa la Bw Kenyatta kunaonekana kama kulipiza kisasi hatua yake ya kumuunga mkono Bw Odinga.
Maandamano zaidi yanapangwa, siku ya Alhamisi wiki hii. Lakini serikali imelaani ghasia na usumbufu unaosababishwa na maandamano hayo.