Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewatoa hofu wapenzi wa timu za Simba na Yanga kwamba fedha alizoahidi kwa kila goli huenda zimeisha akisema fedha hizo bado zipo.
Ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Machi 19, 2023 katika hotuna yake wakati wa shehere iliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) kumpongeza kwa kufikisha miaka miwili madarakani.
Samia aliingia madarakani Machi 19, 2021 baada ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli kufariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitani ya Mzena, iliyopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Katika sherehe hizo zilizofanyikia Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, mkuu huyo wa nchi amezipongeza timu hizo za Simba na Yanga ambazo zinashiriki michuano ya Klabu Bingwa Afarika kwa Simba na Yanga, Kombe la Shirikisho Afrika.
Rais Samia alitoa ahadi kwa timu hizo kuwa kila goli watakalofunga atalizawadia Sh5 milioni.
“Niwapongeze wanangu wa Yanga na Simba kwa kutumia vizuri fursa niliyowapa ya goli moja Sh5 milioni. Wameitumia vizuri sana kwa hesabu nilizonazo Yanga wameshalamba Sh30 milioni na Simba jana Sh35 milioni na huko nyuma nadhani walikula Sh5 milioni,” amesema Rais Samia huku akishangiliwa
“Ni imani yangu ile kasi ya ya milioni tano kwa goli itaendelea hadi fedha hizo zitakapoondoka. Kwa sasa hivi wale waliokuwa wakitania jana kwamba nampigia Msigwa kwamba maliza mpira haraka mimi pesa zimeisha, nataka niwahikikishie kwamba mama bado anazo wekeni mipira kwenye wavu, bado zipo. Jengeni jina la nchi yetu fedha bado zipo,” amesema Rais Samia.
Utani huo ambao Rais Samia ameuzungumzia ni ule wa jana Jumamosi wakati wa mchezo wa Simba na Horoya ya nchini Guinea uliopigwa dimba la Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kwa Simba kuibuka na ushindi wa 7-0.
Ushindi huo uliibuka utani mtandaoni kwa baadhi kuweka picha ya Rais Samia na maneno “Msigwa, mwambie refa amalize mpira, mimi sina hizo hela.”
Gerson Msigwa ni Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye ndiye kila mchezo amekuwa anakwenda na fedha hizo uwanjani ambapo mpira unapomalizika na kama magoli yamefungwa hukabidhiwa papo hapo.
Ushindi huo wa Simba jana Jumamosi, uliiwezesha kufikisha pointi tisa nyuma ya Raja Casablanca ambazo zote zimefuzu robo fainali ya michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika.