RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema watu wasiotaka mabadiliko na mageuzi anayoyafanya kupitia maridhiano, wako ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anariupoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro…(endelea).
Mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, yaliyoandaliwa na Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) na kufanyika leo tarehe 8 Machi 2023, mkoani Kilimanjaro.
Ni wakati akizungumzia mjadala ulioibuka kufuatia hatua Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kumualika kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, ambapo amesema baadhi ya watu walimtuhumu mwanasiasa huyo kuwa amelambishwa asali.
Rais Samia amesema kuwa, changamoto anayokutana nayo Mbowe kutokana na hatua yake ya kukubali siasa za maridhiano, anakumbana nayo ndani ya chama chake cha CCM, huku akitoa mfano kwmba alipopendekeza mikutano ya hadhara iruhusiwe pendekezo hilo lilikuwa gumu kukubaliwa.
“Nilipopendekeza kwenye chama changu tufungue mikutano ya hadhara kulikuwa kugumu kidogo, mjadala ulikuwa mkubwa kama mnavyofanya nyie. Najua juzi Mbowe alikuwa na mjadala mkubwa kidogo kwa nini mlimuita Rais kwenye hili jukwaa, kwa hiyo wahafidhina wako kwangu na wako kwako kidogo,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema “wapo waliomwambia Mbowe ulishalishwa asali, tuambie Ikulu siku ulipotolewa jela ulikwenda kuambiwa nini? Mbona umekuja na lugha hii sasa hivi, akija nje anatandikwa.”
Mwenyekiti huyo wa chama tawala cha CCM, amesema kwa sasa siyo rahisi kwa baadhi ya watu kukubaliana na siasa za maridhiano, lakini watakuja kuzibali baada ya kuona matunda yake, huku akiweka wazi kwamba hakuna kinachoshindikana katika mazungumzo.
“Hali ni kama ilivyo twendeni tukajenge taifa letu, tusibomoe taifa letu. Kwa hali yoyote hakuna kisichowezekana kwenye mazungumzo, tumeshuhudia nchi kadhaa zimeingia kwenye vita hawakupata suluhu, suluhu ilipatikana kwenye mazungumzo. Kwa hiyo tuendelee kuzungumza, najua si rahisi kabisa watu kuja na utamaduni huu mpya ukakubalika mara moja,” amesema Rais Samia.
Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
Rais Samia ameipongeza Chadema kwa kuja na sera yake ya No Hate, No Fear, inayohamasisha wafuasi wake wasiwe na chuki na wala wasiwe na hofu.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amevitaka vyama vya siasa kuendelea kufanya siasa za kistaarabu zenye lengo la kuijenga nchi.
“Panapotokea hoja tukae tuzungumze na si kupayuka kwenye majukwaa tukaanza kushambuliana, hapana. Tusiende tena huko ikitokea hoja viongozi wetu wapo, kaeni kupitia chombo hiki zungumzeni kwa nini hili limetokea liwekwe sawa tuendelee,” amesema Rais Samia.