Rungwe Atoa Mpya, Ataka Wanafunzi na Wagonjwa Wapewe Ubwabwa bure

 


Uongozi wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) umemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuangalia upya mfumuko wa bei hali ambayo inapelekea ugumu wa maisha kwa wananchi, huku mwenyekiti wa chama hicho Hasheem Rungwe akisisitiza suala la chakula shuleni na hospitali linapaswa kutolewa bure.


Wakiongea na waandishi wa habari makao makuu ya Chama jijini Dar es Salaam wanawake hao wameonesha kilio chao kwa Rais huku wakimtaka awakumbuke na wao kwenye nafasi mbalimbali za uongozi.


Mwenyekiti wa Baraza Taifa, Fatuma Seleman amesema yapo mambo mengi yanayomuumiza mwanamke wa Kitanzania ukiachilia mbali mfumuko wa bei, amesema hata katika suala zima la uzazi lazima liboreshwe ili wanawake wakimbilie kujifungulia kwenye vituo vya afya na sio nyumbani.


"Dawa na huduma zingine za kina mama ziboreshwe kwa kiwango kikubwa itasaidia wanawake kujifungua salama," amesema Fatuma.


Merre Mpangala ambaye ni Katibu wa Baraza Taifa amesema serikali inapaswa kuingilia kati suala zima la malezi kwa watoto kwasababu hivi sasa kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili unaosababishwa na malezi mabaya ya wazazi kwa watoto.


"Seikali inapaswa kuingilia kati iweze kudhibiti teknolojia kwasababu ndio chanzo cha kumomonyoka kwa maadili, hizi simu janja (Smartphones) ndio zinaharibu watoto wetu, Serikali inapaswa kushirikiana na wazazi kudhibiti kushuka kwa maadili," amesema Mpangala.


Suala la chakula kama linavyosimamiwa vyema na Chama halikuachwa kuongelewa kwani alipopata wasaa wa kuzungumza Mwenyekiti wa Chama Taifa Hasheem Rungwe amesema suala la chakula shuleni na hospitali linapaswa kutolewa bure.


"Chakula kinapaswa kitolewe bure watoto wetu wanaumia ila hawawezi kuongea wanapaswa wapewe ubwabwa bure, hata katika hospitali wagonjwa wapewe bure kwani Serikali inao uwezo kwasababu inakusanya kodi kubwa," amesema Rungwe.


Mbali na hayo Mwananchi ilitaka kujua ratiba nzima ya chama kwenye mikutano ya hadhara Naibu Katibu Mkuu Taifa, Eugene Kabendera amesema mikutano itaanza mwezi Machi mwaka huu baada ya kikao cha kamati kuu kitakachofanyika hivi karibuni.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad