Ofisi ya Rais wa Russia imewataka maofisa wa nchi hiyo kutotumia simu za iPhone zinazotengenezwa na kampuni ya Marekani ya Apple, kwa sababu kuna wasiwasi kwamba vifaa hivyo vinaweza kuwa hatarini na kutumiwa na mashirika ya ujasusi ya nchi za Magharibi kwa ajili ya kufanya ujasusi.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Russia, Sergey Kirienko, ambaye alikuwa akihutubia kongamano lililoandaliwa na Kremlin kwa maafisa wanaohusika na siasa za ndani, amewataka maafisa hao wabadilishe simu zao ifikapo Aprili mwaka huu.
Ameongeza kuwa: “Kila kitu kimekwisha kwa iPhone, tunapaswa ama kuzitupilia mbali au kuwapa watoto” na kwamba maafisa wote wanapaswa kutekeleza amrii hiyo. Kuna uwezekano kwamba, Kremlin itatoa vifaa vingine na chaguo tofauti kama mbadala kwa iPhone.
Hapo awali, simu za mkononi za viongozi wengi wa nchi na watu mashuhuri, akiwemo Jeff Bezos, mmiliki wa kampuni ya Amazon, na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, zilidukuliwa kwa kutumia programu maarufu ya ujasusi ya Israel, Pegasus.