Dar es Salaam. Wakati Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ukieleza sababu ya ujenzi wa barabara njia nane kutoka Kimara jijini Dar es Salaam hadi Kibaha mkoani Pwani kuchelewa, ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Aprili 15 mwaka huu.
Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 19.2 unaofanywa na kampuni ya ndani ya Estim Constructions Limited ulipaswa kukamilika Januari 2021 kwa gharama ya Sh 141.5 bilioni.
Kuongezeka kwa mkataba mara mbili kulisababisha mkandarasi huyo kuongezewa muda, huku gharama zikibadilika kutoka Sh141 bilioni hadi Sh 218 bilioni.
Akitoa ufafanuzi huo jana wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Rogatus Mativila alisema awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo ilikuwa miezi 30 na ulipaswa kukamilika mwaka 2021.
“Nyongeza ya mkataba ilihusisha upanuzi wa barabara kutoka njia sita hadi nane, ujenzi wa barabara za mzunguko maeneo ya makutano na ujenzi wa maegesho ya malori na kazi yote hiyo iligharimu Sh21 bilioni na muda wa miezi tisa,” alisema Mativila.
Mtendaji huyo alisema wakati ujenzi ukiendelea waliona kunahitajika maboresho, ili barabara iwe na tija na kuondoa kabisa msongamano ambapo ilipendekezwa kuwekwe daraja la juu eneo la Mbezi Mwisho.
“Eneo lingine ni ujenzi wa barabara ya maingilio kwenye stendi kuu ya Magufuli iliyotakiwa kujengwa na Tamisemi, lakini iliigizwa kwenye mradi huu pamoja na stendi ya daladala eneo la Kibamba.
“Pia kulikuwa na kazi ya kuongeza taa za kuongozea magari kwenye maeneo matano, kazi hii imefika asilimia 20, lakini pia taa 460 za barabarani hazijawekwa, ziko kwenye mchakato,” alisema.
Pia alisema nyongeza hiyo ya tatu iligharimu Sh57 bilioni na kubadilisha gharama nzima ya mradi kutoka Sh161 bilioni ya nyongeza ya pili hadi kufikia Sh218 bilioni na muda wa mradi kuongezwa kwa miezi 18, sasa ukitarajiwa kukamilika Aprili 15 mwaka huu.
Alibainisha baadhi watu kuvamia maeneo ya hifadhi ya barabara na kuchelewa kuwasili kwa taa kutokana na janga la ugonjwa wa Uviko 19, pia vimechelewesha mkandarasi na kwamba mradi huo umefikia asilimia 98. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Selemani Kakoso aliishauri Tanroads kuangalia namna ya kupunguza gharama kwa kutumia wataalamu wa manunuzi ili waweze kuwasaidia.
Alisema katika miradi mingi wanayoitekeleza huanza kwa gharama ndogo, na inapomalizika huwa na gharama kubwa huku akiwataka kubuni vyanzo vya mapato vitakavyowasaidia kwenye matengenezo.
“Angalieni namna mtakavyoanzisha barabara zenye tozo, ili kuwaongezea mapato. Sheria inaruhusu kama kuna njia mbadala anzisheni, mfano daraja la Tanzanite ni mojawapo kama mtu hawezi kupita Selander basi alipie,” alisema Kakoso.
Akizungumzia suala la miundombinu ya maji, aliwataka Tanroads kuiimarisha na kila wanapojenga wawe na mipango mizuri, mvua zitakaponyesha wananchi wasidhurike kwa kuwa yapo baadhi ya maeneo yamenyanyuliwa, wananchi wanaoishi chini wanaathirika.