Sakata la Feisal Toto Tunajitekenya na Kucheka Wenyewe

 

Sakata la Fei Toto

Achana na zile propaganda za mama yake Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwamba Fei alikuwa akila ugali kwa sukari pale Yanga. Ni propaganda za ajabu hivi.


Sijui ni nani alimwongopea mama yale maneno. Ameongea yeye ila aibu naona mimi. Uongo mtupu.


Yawezekana Fei alikuwa na changamoto lukuki pale Yanga. Ni kawaida. Watu wengi hupata changamoto katika maeneo yao ya kazi.


Si ajabu kama Fei Toto alipata changamoto hizo pale Yanga. Ila alichozungumza mama yake alikuza sana mambo. Ni wazi kabisa.


Ni kweli Fei kwa utumishi wake pale Yanga alistahili maisha mazuri zaidi. Huyu ndiye alikuwa kioo cha timu.


Fedha aliyokuwa akilipwa na Yanga ni kidogo ukilinganisha na uwezo wake uwanjani. Walipaswa kumpa zaidi. Kwanini hawakumpa? Wanajua wenyewe.


Kinachowauma wachezaji aina ya Fei ni kuona kuwa wameishika timu, lakini pesa wanapewa kina Bernard Morrison na Stephane Aziz Ki ambao wana mchango mdogo kuliko yeye. Inaumiza sana.


Sasa wiki hii tumeona Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ikitupilia mbali marejeo ya kesi yake dhidi ya Yanga.


Kwa maana hiyo kamati imesema Feisal bado ni mchezaji halali wa Yanga. Ni vilevile kama walivyoamua Januari 9, mwaka huu. Hakuna kilichobadilika.


Hapa ndipo kichekesho chenyewe kinapoanzia. Kwanza kama walivyofanya awali, kamati imekuwa na haraka katika uamuzi wake. Walikuwa na ulazima gani wa kutoa taarifa nusu nusu kama mwanzo? Hakuna!


Kamati ingekaa na kumaliza hukumu yote kisha itoe taarifa ikiwa imekamilika. Siyo hivi vipeperushi vya kila siku. Ila kwa sasa tuachane na hilo. Tuzungumze kuhusu hatima ya Fei.


Ni wazi kuwa Feisal ameshaamua kuwa hataki kuichezea tena Yanga. Hataki na hilo wala halina kificho.


Kama Fei Toto angekuwa bado anaitaka Yanga angesharejea tangu Januari, lakini hataki na amesimamia hilo kidete.


Hili ndilo ambalo TFF walipaswa kuliona. Ili kuokoa kipaji cha Feisal walipaswa kuangalia namna ya kuvunja mkataba wake na Yanga. Haya mengine ni siasa tu sawa na kujitekenya kisha kucheka mwenyewe.


Haijalishi TFF wanaamua nini ukweli unabaki palepale kuwa Fei Toto haitaki tena Yanga. Kwanini wanamlazimisha?


Kanuni za Fifa ziko wazi kabisa. Mchezaji sio mtumwa na hapaswi kulazimishwa kuichezea timu fulani. Awe na sababu ya msingi au la, ila hapaswi kulazimishwa.


Kwanini Kamati ya TFF inamlazimisha Fei Toto abaki Yanga? Wanajua wenyewe. Mbaya zaidi wanafahamu wazi kuwa Fifa inakataza hilo. Ila wameamua kufanya wanavyojua wenyewe.


Haijalishi hili sakata linakwendaje ila mwisho wa siku ni wazi kuwa huu mkataba utavunjika kwasababu upande mmoja wa mkataba ulishakataa kuendelea nao.


Kinachofanyika sasa ni siasa tu na kuchelewesha mambo. Ila mwisho wa siku Fei Toto ataondoka Yanga na mkataba utavunjika.


Haijalishi utavunjwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhisi wa Michezo (CAS) au Fifa ila kwa wanaofuatilia kanuni za soka duniani wanajua kuwa utavunjika tu. Kwanini tunalazimisha mambo kwa sasa? Inashangaza sana.


TFF iwaite Yanga na Fei mezani ivunje huu mkataba kwa maslahi ya pande zote mbili. Hakuna haja ya kuacha mambo yaende mbali sana wakati hatima yake inafahamika.


Fei atakuwa karejea uwanjani na kuendeleza kipaji chake. Na TFF wanapaswa kuhakikisha hilo. Wanafahamu kabisa kuwa Fifa inataka wachezaji wacheze. Ndio kipaumbele cha soka.


Hivyo kwa sakata hili la Fei Toto tunamchelewesha tu mchezaji wa watu. Tunajitekenya tu na kucheka wenyewe.


Lakini kama msimamo wa Fei haubadiliki basi hawezi kurudi Yanga daima. Sio TFF wala Yanga wanaweza kumlazimisha. Hawezi kurudi.


Swali kubwa hapa ni kwamba kwanini Fei amekuwa na msimamo huu licha ya umuhimu wake pale Yanga?


Anafahamu vyema alichopitia pale Yanga. anafahamu vyema mchango wake pale Yanga. Kwanini hataki kurudi Yanga? Anajua vyema yeye.


Ila ni wazi kuwa kwa umri wake Fei anafahamu wazi kuwa kwa sasa anatakiwa kupata pesa zaidi kutoka katika kipaji chake. Pengine ameona hawezi kuipata Yanga. Anajua anakoweza kupata.


Pengine aliwapa Yanga fursa ya kutosha kumpa hiyo keki na hawakuweza hivyo ameona akatafute kwingine. Ni maisha yake hivyo ana uamuzi katika hilo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad