Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepiga marufuku wanafunzi wa kuanzia madarasa ya awali hadi darasa la tano kusoma shule za bweni (boarding).
Kupitia waraka uliotolewa na Kamishna wa Elimu wa Wizara hiyo, Dk. Lyabwene Mtahabwa kwa wadau wa elimu nchini, serikali imezitaka shule zote zinazotoa huduma ya bweni kwa madarasa ya kwanza hadi la tano kusitisha huduma hiyo ifikapo mwisho wa muhula wa kwanza mwaka 2023.
Dk. Mtahabwa amesema hairuhusiwi kutoa huduma ya bweni kwa wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza isipokuwa kwa kibali maalum kitakachotolewa na Kamishna wa Elimu baada ya kupokea maombi kutoka mdau husika na kwamba utekelezaji wa waraka huo umeanza Machi 1, 2023.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa mwongozo wa uanzishaji wa usajili wa shule uliotolewa na wizara Novemba 2020.