SERIKALI imeanza kutafuta ufumbuzi wa kupunguza tatizo la ajali zinazotokea mara kwa mara kwenye Mlima Sekenke ulioko Iramba mkoani hapa.
Ajali hizo zimekuwa zinachangiwa na miteremko na kona kali zinazokatiza kwenye madaraja ya kina kirefu na kusababisha madereva wengi kushindwa kumudu magari yao eneo hilo la barabara kuu ya Singida-Shelui-Nzega, mkoani Tabora.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Singida, Msama Msama alisema hayo jana alipowasilisha taarifa ya utekelezaji miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2022/23 katika kikao cha 46 cha Bodi ya Barabara.
Alisema barabara hiyo ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami mwaka 2008, ikiwa ni miaka 15 sasa, imekuwa inatumika na magari mengi yakiwamo ya uzani mkubwa, hali inayohitaji matengenezo kutokana na kuharibika.
Msama alisema hadi sasa Mhandisi Mshauri anaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara hiyo, akisimamiwa na TANROADS Makao Makuu na kazi hiyo imefikia asilimia 75.
Alimtaja Mhandisi Mshauri aliyepewa kazi hiyo kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 1.22, M/s Intercontinental Consultants and Technocrats Pvt. Ltd in JV, M/s Advanced Engineering Solution Ltd in association na M/s Intercontinental Consultants and Technocrats Co. (T) Ltd
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega alisema ili kumaliza tatizo la ajali eneo hilo, ni lazima jamii ishirikishwe kupata suluhisho la kudumu.
"Serikali ilijenga barabara mpya ikaachana na ile ya zamani iliyokuwa inasababisha ajali, sasa tulidhani tumemaliza tatizo, lakini bado ajali zinatokea.
"Tujenge upya tena kwenye eneo hilo, kuna haja sisi Wanyiramba tukafanye jambo letu la asili pale," Mkwega alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda alisema suluhisho la ajali maeneo hayo ni kuukwepa mto kwa kupasua upya barabara pembezoni mwa mlima ili kupunguza wingi wa madaraja na kona kali.
Kuhusu kauli ya kushirikisha Wanyiramba, Mwenda alisema kwa sasa jamii hiyo imeshastaarabika na wala haijishughulishi na masuala hayo.
Mwenyekiti wa kikao ambaye ni Mkuu wa Mkoa huo, Peter Serukamba aliwataka viongozi na watendaji wa umma mkoani humo kushikamana pamoja ili kusimamia miradi badala ya kupigana majungu na kukwamisha maendeleo kwa wananchi.
Alisema kazi nzuri zinazotekelezwa kwa ufanisi na baadhi ya sekta zinatakiwa kuungwa mkono badala ya kusemana na kupeana taarifa ambazo siyo sahihi.